KINYUA BIN KING’ORI: Raia wawe macho wasichague waliowaahidi hewa

KINYUA BIN KING’ORI: Raia wawe macho wasichague waliowaahidi hewa

NA KINYUA BIN KING’ORI

WANASIASA wamejaa mashinani wakati huu, wakizunguka usiku na mchana mitaani na mazishini wakikutana na wananchi kuwaelezea nia zao kugombea nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wengi wanatoa ahadi za yale wanayoazimia kutekeleza iwapo watachaguliwa, ila kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya ahadi hizo hata haziwezi kutekelezeka.

Wengi wanatoa tu ahadi hizo kwa lengo la kujivumisha mashinani na si kuboresha maisha ya wapiga kura wakipata uongozi. Wengine wanaowania nyadhifa za udiwani, ubunge, useneta na kadhalika wanatoa ahadi tu lakini hawawezi kuelezea wananchi mikakati watakayosuka kuzitekeleza wakichaguliwa.

Wanaahidi mambo ambayo hawana uwezo kwayo au hayamo miongoni mwa majukumu yao kikatiba. Wananchi wanafaa kuwa makini wasije kupotoshwa na wawaniaji hao.

Inafaa kila mgombezi kujieleza atakavyoweza kuinua maisha ya wapiga kura kwa kuzidisha miradi na kuboresha uchumi kwa maslahi ya umma.

Kwa sasa wagombeaji wengi wanaozunguka kuomba kura hawana mawazo ya kujenga taifa wala mbinu kuwasaidia wananchi bali wanataka tu kuchaguliwa kujifaidi kwa mamlaka hayo makubwa wakilipwa pesa nyingi.

Jiulize, je, ikiwa wanaelewa majukumu yao katika nyadhifa wanazotaka kugombea, kwa nini hawatuvutii kwa sera bali kulalamika na kulaumu viongozi wanaoshikilia nyadhifa hizo kwa sasa kwa kushindwa kutekeleza ahadi zao kwa nia ya kuimarisha maendeleo mashinani?

Viongozi hao watarajiwa wakome porojo na uzushi wawe wajasiri kujipangia mikakati na sera kuvutia wapiga kura. Ni unafiki kwa wananchi kukubali kutumiwa na wanasiasa kwa kuwachekesha tu na kuwauzia porojo na propaganda badala ya kuthibitisha ubora wa mawazo yao kuendesha siasa kwa sera.

Hata wengine, wanaingia mitaani kwa ahadi hewa na wananchi wanawasikiliza tu bila kuwauliza maswali. Hebu, niulize mgombezi wa wadhifa wa ubunge anayejipiga kifua kwa ahadi anaweza kuwaajiri vijana, kujenga masoko, kuwezesha wafanyibiashara kunufaika zaidi na hata kuwatafutia matibabu wagonjwa ikiwa atachaguliwa mbunge wa eneo fulani kijijini, anafaa kuchaguliwa bungeni 2022?

Viongozi watarajiwa wanafaa kufahamu fedha zinazotengwa katika nyadhifa wanazowania. Kwa mfano huwezi kusema kile utafanikiwa kufanyia wakazi wa eneo la Voi ukichaguliwa mbunge wakati hauna habari kuhusu kiasi cha fedha kinachotengewa hazina ya kustawisha maeneobunge ujui NG-CDF na kujua ni Miradi ipi zinazofaa kutekeleza.

Wananchi wakielewa wajibu wa kila kiongozi mapema, wataweza kuwachuja wanatoa ahadi hewa mapema.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Wanawake ni thawabu kuu tunayofaa kujivunia

Munya atangaza kupigania ugavana Meru