KINYUA BIN KING’ORI: Tumefanya uamuzi wetu kwenye debe, sasa turudi kazini tujenge nchi

KINYUA BIN KING’ORI: Tumefanya uamuzi wetu kwenye debe, sasa turudi kazini tujenge nchi

NA KINYUA BIN KING’ORI

HATIMAYE, tumepata viongozi wapya na wanasiasa wengine mashinani wanashangilia baada ya kutangazwa washindi, wengine roho juu wakisubiri matokeo kutangazwa huku waliopoteza katika uchaguzi huo wakiwa kwenye huzuni na masikitiko tele.

Hata hivyo, tujue washindi na washinde wote ni Wakenya na waliochaguliwa wametwikwa jukumu zito la kuwatumikia raia wote bila kujali ikiwa walikuwa wafuasi au mahasimu wao katika kampeni.

Pia, itakuwa vyema sote tusahau chuki,uhasama ,mkwaruzano na tofauti zetu zilizotukumba kipindi cha kampeni tudumishe upendo, umoja na amani tukiwa jamii moja.

Ushauri wangu kwa viongozi wapya, huu ni wakati wa kuthibitisha kweli walistahili kuchaguliwa kwa kuanza kushirikisha umma kupanga mikakati ya maendeleo punde tu wakiapishwa, kushirikisha na kuwaunganisha wananchi wote itakuwa busara kwao.

Aidha, kwa sababu kampeni zilikuwa zimekwamisha shughuli zetu za ujenzi wa taifa kote nchini, huu ni wakati wa kurejelea shughuli za kawaida kwa bidii ya mchwa ili kuchangia ustawi na maendeleo ya taifa.

Siasa ziliteka nyara hata biashara kiasi cha unga wa Sh100 kufichwa na walaghai.

Wakenya wanafaa kujua hatari ya kukubali kutumiwa na wanasiasa walioshindwa kuendelea na siasa kusuta wapinzani.

Badala yake, watumie nguvu zao kuhakikisha wamejituma kujiruzuku kimaisha.

Kazi zao ndizo muhimu kwa sasa.

Tunaomba wote ambao hawajaridhika na matokeo wawe watulivu kwa kutumia taratibu zilizowekwa kufika kortini.

Hivyo, tumepiga kura na kuchagua viongozi watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano, siasa ziishe tuwape nafasi kutekeleza ahadi bila usumbufu na sisi tuwe na muda kujenga maisha na taifa letu tukiwa kazini.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Jinsi Kiswahili kilivyotumiwa na wanasiasa...

Mwanamke anyakwa akiwa na manoti kituoni

T L