KINYUA BIN KING’ORI: Tusipuuze athari za corona hata tukipokea chanjo

KINYUA BIN KING’ORI: Tusipuuze athari za corona hata tukipokea chanjo

NA KINYUA BIN KING’ORI

NI mwaka mmoja sasa tangu kisa cha kwanza cha homa hatari ya corona kuthibitishwa humu nchini.

Mataifa mengi ulimwenguni Kenya ikiwemo yamejitahidi kuwekea raia wao masharti makali ya kuzingatiwa kuzuia msambao wa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Juhudi zingine zinazostahiki kupongezwa ni wataalamu wa afya kwa ushirikiano mkubwa na Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) kufaulisha kupatikana kwa chanjo ya maradhi hayo ya kuambukizana. Tayari baadhi ya Wakenya hasa wahudumu wa afya wameanza kupokea chanjo ya Astrazeneca.

Kwa kuzingatia jinsi Covid-19 imetishia maisha kwa kuendelea kuangamiza maisha ya watu wengi ulimwenguni, serikali inapaswa kuhakikisha wananchi kuanzia mashambani na mijini wamechanjwa bila kujali umri, viwango vya elimu au imani yao.

Hatusemi chanjo hiyo ndiyo tiba ya corona, bali ni mojawapo ya mbinu bora kwa mtu kudhibiti maambukizi.Pongezi kwa baadhi ya vinara wa kaunti ambao tayari wamejitokeza kuchanjwa miongoni mwao akiwa Gavana wa Taita Taveta, Granton Samboja na Prof Kivutha Kibwana wa Makueni.

Vitendo vyao vimeonyesha ushujaa wao na wananchi wengi sasa wamepata pia ujasiri wa kutaka kupokea chanjo hiyo. Ni wajibu wa serikali kusambaza chanjo hiyo kote mashinani kuwezesha kila mtu kuipokea bila usumbufu tena iwe bila malipo.

Siku za hivi karibuni, tumeanza kushuhudia ongezeko kubwa la maambukizi ya COVID-19, kumaanisha ugonjwa huo ungali unasambaa mno na hatuna budi kujichunga kwa kuzingatia masharti yanayotolewa na serikali kupitia wizara ya afya.

Majuzi Rais Uhuru Kenyatta akihutubia Taifa, alizidisha masharti mapya kwa kuwapiga breki wanasiasa kufanya mikutano ya kisiasa kwa muda wa mwezi mmoja huku kafyu ikirefushwa kwa miezi miwili zaidi.

Ukweli ambao Rais uhuru, anafaa kuambiwa ni kwamba agizo lake huenda likose kuzaa matunda ikiwa maafisa wa usalama watakuwa waoga na kutekeleza agizo hilo kwa mapendeleo.

Lisilopingika kama mchana wa jua ni kwamba, viongozi wa kisiasa kutoka mirengo yote, kuanzia Rais Kenyatta, Naibu wake Dkt William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Mwenyekiti wa KANU, Seneta Gideon Moi, magavana miongoni mwa wengine, wanapaswa kulaumiwa kwa kukosa kujitolea kikamilifu kuzuia msambao wa janga la corona nchini.

Ikiwa wanasiasa wataendelea kuvunja masharti yaliyowekwa na serikali kwa kutokomesha mikutano yao ya kisiasa kwa kipindi hiki cha chanjo ya maradhi hayo, watakosea na inafaa wawajibishwe kudhibiti msambao wa corona.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tujuzwe sababu za bei ya mafuta kupanda kila...

Magavana Kenya wamwomboleza Rais Magufuli