KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa eneo la Nyanza waitikie wito wa kufanya kazi na Rais Ruto

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa eneo la Nyanza waitikie wito wa kufanya kazi na Rais Ruto

VIONGOZI nchini wajue siku zao uongozini zilianza kuhesabiwa mara tu walipoapishwa kutwaa nyadhifa zao.

Katika kutekeleza majukumu yao ni lazima washirikiane na viongozi wengine bila kujali mirengo yao kisiasa, ili kutimizia wananchi ahadi walizotokea kwenye kampeni.

Wakianza kujitenga itakuwa kuchukua mwelekeo usiofaa ilhali wananchi wameacha siasa na kuzamia shughuli za ujenzi wa taifa.

Hulka kama hii ni hatari kwani huenda wakawa kizingiti kwa juhudi za maendeleo kufikia wananchi maeneo husika.

Katika uchaguzi uliopita Wakenya walichagua viongozi kutoka mirengo yote.

Hivyo, viongozi wakubali kufanya kazi kwa pamoja bila kujitenga, kuogopa wala kuongozwa na mihemko ya siasa. Siasa za ubinafsi ni adui wa maendeleo.

Muhimu ni nchi isonge mbele.

Huu ni wakati viongozi wa Nyanza, hususan waliochaguliwa kupitia ODM, wakubali kushirikiana na serikali ya Rais William Ruto kuboresha maendeleo eneo hilo.

Japo si lazima kiongozi ashirikiana na rais wa nchi ili kutimiza ahadi alizowapa wapigakura wa eneo lake, ushirikiano utaimarisha juhudi za kuhakikisha maendeleo yanayoratibiwa na serikali ya kitaifa yanasambazwa kwao bila ubaguzi au vikwazo.

Kuna ahadi, hususan ujenzi wa miundomsingi mikuu, ambazo viongozi watafanikisha kwa urahisi iwapo watakuwa katika meza ya mazungumzo ya maendeleo ya kitaifa.

Kwa hilo kufaulu itabidi washirikiane na serikali ya kitaifa na Rais Ruto.

Wananchi wa Nyanza hawakufanya kosa lolote kuunga mkono kinara wa Azimio, Raila Odinga, katika uchaguzi wa Agosti walitimiza wajibu wao kikatiba.

Wana haki kufurahia matunda ya serikali ya kitaifa sawa na Wakenya wengine. Rais Ruto amejitolea kushirikiana na viongozi wote kuleta maendeleo.

Itakuwa ukomavu kwa viongozi wa Nyanza kuitikia wito huo wenye nia njema.

Kukosa ushirikiano baina ya Rais na viongozi wa mashinani mara nyingi hukwamisha maendeleo au kuacha baadhi ya maeneo, hasa ngome za upinzani, kubaguliwa katika miradi.

Hata hivyo, Rais Ruto amejitolea kushirikiana na viongozi wote kwa manufaa ya maendeleo. Hivyo, itakuwa ukomavu viongozi wa Nyanza waitikie wito huo wenye nia njema.

Mnamo Jumapili, wakazi wa mjini Homa Bay walithibitisha ukomavu wao kwa kumpokea kwa shangwe Dkt Ruto alipozuru kaunti hiyo; tunarajia viongozi wao wataungana na Rais atakaporejea tena katika ziara ya maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Magavana wajitolee kugawia manaibu...

Hofu njaa kuleta vurugu za kijamii

T L