KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa Jubilee wasipuuze maoni ya wanachama

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa Jubilee wasipuuze maoni ya wanachama

Na KINYUA BIN KING’ORI

UMAARUFU wa chama tawala cha Jubilee unakabiliwa na tishio kubwa baada ya chama hicho kushindwa katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kiambaa.

Eneobunge hilo lipo katika ngome ya Rais Uhuru Kenyatta, lakini hali ilivyo, chama kimeendelea kufifia maeneo ya Mlima Kenya, huku Uchaguzi Mkuu wa 2022 ukikaribia.

Kilichojiri katika uchaguzi huo mdogo huenda kilitoa taswira ya hali halisi ya jinsi mambo yalivyo mashinani, hasa kwa upande wa viongozi waliopo Jubilee ambao wamekuwa wakiwasuta wenzao wanaotaka masuala ya kiuchumi na urithi, kuhusiana na eneo la Mlima Kenya kushughuliwa.

Wakazi wa Kiambaa walitoa ujumbe mzito kwa kiongozi wa taifa na chama chake kwamba kuafikia baadhi ya maamuzi muhimu chamani, si wajibu wa kiongozi mmoja au wawili pekee, bali wanachama wanapaswa kushirikishwa kwa masuala yote muhimu kabla ya kutekelezwa.

Kushindwa kwa chama hicho ni sawa na Rais uhuru Kenyatta kupigwa dafrao kisiasa na naibu wake.Maswali mengi yanaibuka baadhi yakiwa ni vipi wananchi ambao wameishi kushabikia chama fulani na kiongozi wake wakubali kukumbatia sera za mgombezi wa chama kingine?

Je, mbona wakazi wa Kiambaa waliotarajiwa kumpigia kura kwa wingi Bw Kariri Njama wa Jubilee, wavunje itikadi hiyo na kumpigia kura mwaniaji wa UDA, Bw Wanjiku? Hayo ni mabadiliko katika siasa zetu 2022 ikiwa viongozi wa vyama vikuu nchini watakosa kusikiliza malalamishi ya wanachama wake na kuamua kufanya watakavyo bila kujali raia watakaowaonyesha makali yao kwa kuwachagua viongozi wa vyama vingine vidogo bila kujali ikiwa anayehusishwa na chama hicho ni nani.

Ushindi huo sasa utaamsha Jubilee kutoka usingizini na kukubali kushughulikia matatizo yanayokumba wanachama na chama kwa jumla.Wanachama wangependa kuhusishwa hasa katika masuala ya uchumi ambao umekuwa mzigo mzito, kutengwa na kudharauliwa kwa Naibu Rais Dkt William Ruto, kushirikiana kwa Rais na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Pia wanachama wangependa zaidi kuelewa kuhusu ushirikiano wa Rais na Bw Odinga na fununu kwamba atamuunga mkono kiongozi huyo wa ODM katika uchaguzi wa 2022. Licha ya kutumia fedha nyingi, chama hicho kimekuwa kikishindwa katika chaguzi ndogo nyingi ambazo zimefanyika nchini.

Viongozi wa Jubilee wanafaa kuandaa kongamano la kitaifa wajadiliane mustakabali wa chama, umoja wa taifa, usalama, kumaliza ukabila na hali ya kiuchumi inayomlinda mwananchi wa kawaida.

  • Tags

You can share this post!

Kiongozi wa upinzani TZ azuiliwa usiku wa manane

Bodaboda wahalifu wadhibitiwe haraka