KINYUA BIN KING’ORI: Wawaniaji wenza sasa wathibitishe umaarufu na uwezo wao katika siasa

KINYUA BIN KING’ORI: Wawaniaji wenza sasa wathibitishe umaarufu na uwezo wao katika siasa

NA KINYUA BIN KING’ORI

HATIMAYE wawaniaji wawili wakuu wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, Bw Raila Odinga wa Azimio la Umoja-One Kenya na Naibu Rais Dkt William Ruto wa Kenya Kwanza wamevuka ‘viunzi’ vya kisiasa kwa kuwateua wagombea wenza wao.

Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua ndiye mgombea mwenza wa Dkt Ruto huku Bi Martha Karua akiwa wa Bw Raila.

Licha ya wanasiasa hao kuteuliwa katika nyadhifa hizo muhimu, watarajie mtihani mgumu wa kuthibitishia wafuasi wa miungano yao kwamba watawanufaisha kwa kuwaletea kura nyingi kutoka ngome zao hasa ikizingatiwa wote wanatoka katika eneo la Mlima Kenya lenye idadi kubwa ya wapigakura.

Mwaniaji mwenza ni kiongozi ambaye anafaa kuwa na sifa sawa na mwaniaji urais ambaye anaweza kuaminika kusongesha mbele nchi hasa kiuchumi, kisiasa, kidemkorasia na kiustawi kwa jumla.

Teuzi zao zinafaa kubadilisha joto la kisiasa nchini kwa kuzidisha umaarufu katika mirengo hiyo. Hata hivyo, wanapotekeleza wajibu wao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuchangia amani, umoja na udugu kwa kuepuka matamshi na mienendo yenye kuchochea vurugu na ghasia katika uchaguzi ujao.

Wagombea wenza wote lazima wajitokeze kuelezea mikakati yao kuhakikisha wakubwa wao watatimiza ahadi kwa raia wakichaguliwa kuwa rais kwa kutimiza sera zao.

Wajitokeze kama suluhu au dawa mujarabu ya kukwamua miradi iliyokwama, kusaidia kurejeshwa kwa fedha za umma zilizoporwa na kufichwa mataifa ya nje, kurejeshea taifa hadhi kwa kufaulisha vita dhidi ya ufisadi na kadhalika.

Japo umaarufu wao utachangia pakubwa katika ushindi, wajue taifa hili linahitaji kuongozwa kwa usawa wa kisheria kwa kukuza demokrasia na usambazaji wa ajira bila ubaguzi wa kisiasa au kikabila.

Wakitwaa mamlaka, wathibitishe ukomavu kwa kutatua matatizo yanayowasumbua Wakenya katika sekta hasa za afya , elimu, kilimo na kiuchumi.

Wawaniaji wenza tunayo imani watakuwa viongozi wanaoweza kunyenyekea na kushauriana na wakubwa au wadogo wao serikalini kwa njia ya heshima bila kuvutia malumbano na uhasama tunaoshuhudia nchini kwa sasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto.

Utawala wa Azimio au kenya kwanza utasifiwa au kukosolewa kutokana na namna Rais, Naibu wake na wahusika wengine watakavyojitolea kubadilisha uchumi wetu kwa manufaa ya raia wote wakishindwa Urais Agosti 9, 2022.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Juhudi za kuzima uhalifu zisiwe...

Rais Kenyetta amsimamisha kazi Jaji Chitembwe

T L