KINYUA KING’ORI: Serikali itathmini upya mpango wake wa kuagiza mahindi ya GMO nchini

KINYUA KING’ORI: Serikali itathmini upya mpango wake wa kuagiza mahindi ya GMO nchini

NA KINYUA KING’ORI

HATUA ya serikali ya Rais William Ruto kuagiza mahindi yanayokuzwa kwa njia ya kisayansi (GMO) kwa lengo la kudhibiti baa la njaa nchini huenda isiwafaidi wengi kwa hofu ya kuhatarisha maisha yao.

Serikali imepanga kuagiza mahindi hayo kutoka ughaibuni kwa kipindi cha miezi sita, jambo ambalo limetia tumbojoto baadhi ya wanasiasa na wakulima wa mahindi, hasa kutoka Bonde la Ufa.

Raia wamechanganyikiwa wasijue wazingatie ushauri upi. Huku serikali ikisifia, viongozi mbalimbali wakiwemo wa upinzani wamejitokeza kupinga hatua hiyo. Ingawa ni wajibu wa serikali kuhakikisha Wakenya wanaopitia changamoto maishani yakiwemo makali ya njaa wanapata matumaini ya kuishi kesho, raia wanafaa kushirikishwa kutoa maoni au mapendekezo kuhusu hatua zozote zinazochukuliwa kwa manufaa yao.

Raia watachukuliaje swala hili wakati Waziri wa Biashara Moses Kura analizungumzia kimzaha badala ya uzito unaostahili? Mbona Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi amesalia kimya wakati huu mjadala wa GMO umeshika kasi nchini?

Kati ya Waziri wa Biashara na Waziri wa Kilimo ni nani mhusika mkuu katika swala hilo? Wananchi wamepitia mengi kuanzia janga la Corona, ukame, uchumi kudorora na njaa na GMO isiongezwe katika orodha ya matatizo yao. Wakenya hawana haja na siasa za mahindi au makabiliano yasiyo na maana.

Kile tunauliza ni kwa nini serikali iwe na pupa kutekeleza mpango huo bila mashauriano ya kina? Je,wakulima wetu wanaotarajia kuvuna mahindi yao mapema mwakani watapata soko wapi ikiwa mahindi ya GMO yatakuwa mengi nchini?

Serikali imeanza kuonyesha ujeuri kwa wakenya kiasi cha kutosikiliza maoni yao na itakuwa dharau kuu ikiwa itaendelea kusonga mbele kutekeleza hatua hiyo bila maelewano ya kuridhisha. Vinginevyo, Wakenya watabakia kuamini uvumi kwamba utawala wa sasa huenda unashikinizwa na mataifa ya kigeni kuondoa marufuku dhidi ya GMO kwa manufaa yao.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uhispania wabebesha Costa Rica...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ubelgiji watolewa jasho na Canada...

T L