KINYUA KING’ORI: Vikao vya Raila kutetea makamishna wa IEBC ni mzaha mtupu

KINYUA KING’ORI: Vikao vya Raila kutetea makamishna wa IEBC ni mzaha mtupu

NA KINYUA KING’ORI

TANGAZO la Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kufanya misururu ya mikutano katika ngome zake kama hatua ya kutetea makamishina wanne wa IEBC wanaochunguzwa na kamati ya Bunge kwa madai ya kukiuka maadili ni sarakasi na mzaha tupu.

Makamishina hao – Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya huenda – wakatimuliwa ikiwa mchakato unaoendelea kwa sasa utazingatia sheria hadi mwisho.

Kiongozi wa Azimio na ODM Raila Odinga amechelewa kuwaokoa Makamishna hao hasa ikizingatiwa wabunge wa Azimio walijiondoa katika vikao vya kamati ya kuwachunguza ambapo wangepata nafasi bora kuwatetea na kujiondoa kwao ilikuwa ishara ya usaliti mtupu.

Hivyo, mikutano ya hadhara ya Raila haina nia njema. Huenda ikatumiwa kugawanya Wakenya na kupalilia chuki. Ikiwa Raila alishindwa kutumia wabunge wake Bungeni, mpango huo wa kutembea katika ngome zake akifanya mikutano wakati huu Wakenya wanakabiliwa na njaa utaumiza raia zaidi maana watatumia muda wao mwingi kuhudhuria mikutano hiyo badala ya kujihusisha na shughuli zao muhimu kujenga taifa na kujitafutia riziki.

Wanasiasa ni wajanja. Wanataka kutumia mikutano hiyo kama mbinu ya kuendeleza ajenda zao kisiasa huku wakijifanya kutetea maafisa hao wa IEBC.

Kitendo cha vinara wa upinzani kuacha Cherera na wenzake kukaangwa na wabunge ni funzo kwa maafisa serikalini kuepuka kuhusishwa na wanasiasa wakiwa katika shughuli rasmi kutekeleza majukumu yao.

  • Tags

You can share this post!

JURGEN NAMBEKA: Vijana watangamane na wanaowafaa msimu huu

Takriban raia wa Uganda 46 hufariki kwa Ukimwi kila siku

T L