Habari Mseto

Kioja cha mwaka mwanamume kwenda haja kubwa kitandani kwa mpango wa kando

November 1st, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME mmoja kutoka mjini Bura, kaunti ya Tana River aliwaghadhabisha wakazi na kuwasababisha kumpa kichapo cha mbwa koko, baada ya kwenda haja kubwa katika kitanda cha mpango wake wa kando.

Jamaa huyo aliyebainika kwa jina Mwata aligutushwa Alhamisi asubuhi na maji baridi aliyomwagiwa yakifuatwa na viboko vya makalio na wakazi waliokuwa na hasira, baada ya mpenzi wake aliyeraushwa na harufu mbaya, na kupata kuwa jamaa alikuwa amejisaidia haja kubwa kitandani kumwitania.

Jamaa huyo anadaiwa kuwa alikuwa amempeleka burudani mpenzi wake huyo kwa jina Dorothy Mueni suiku wa Jumatano ambapo alibugia pombe kupita kiasi.

Bi Mueni aliamua kumpeleka Bw Mwata nyumbani kwake wakalale huko, japo ana familia.

“Tulitembea tukinywa nao, alikuwa akilipa bili na alikuwa amempa mwanamke huyo pesa fulani pia alipie endapo angelewa sana. Baadaye alianza kuvurugana na watu na ndipo mpenzi wake aliamua kumpeleka nyumbani,” rafikiye Bi Mueni akasema.

Mwata anasemekana kuwa mlevi zaidi usiku huo kiwango cha kumfanya mpenzi wake kutafuta Bodaboda ya kuwabeba hadi nyumbani kwake, ambapo pia ni karibu na nyumbani kwa familia ya yake.

Rafikiye huyo, ambaye hakutaka kutajwa alisema kuwa wawili hao wamekuwa katika uhusiano huo kwa miezi minne sasa, licha ya kufahamu kuwa mwanamume huyo ni mume wa mmoja wa wateja wake katika saluni anayomiliki.

Alisema kuwa mume huyo amekuwa akimtembelea mpango wake wa kando saa za usiku ama wakati mkewe ametembea nyumbani kwao mashambani.

Wakati mwingine mwanaume huyo anasemekana kumhadaa mkewe kuwa anasafiri nje ya mji, lakini anaishia kwenda kwa Bi Mueni kujiburudisha.

Mwanamke huyo naye pia anasemekana kuwa katika uhusiano na afisa wa polisi aina ya AP ambaye anafanya kazi mbali na mji huo.

Alhamisi, Bi Mueni aliamka saa kumi usiku baada ya kuhisi harufu mbaya zaidi katika chumba chake, ndipo akabaini kuwa mwanamume huyo ambaye “alikuwa amejilaza kama mfalme kitandani” alikuwa amekunya.

“Nilimsikia akifoka kwa hasira na kumtusi mwanaume huyo ambaye hakuwa akijibu kwa kuwa alikuwa amelala. Nilipofika, nilimpata akijaribu kung’oa miwa kwenye ua,” akasema rafiki huyo.

Dorothy anasemekana kumwagia mwanaume huyo maji baridi kwa hasira kisha akaanza kumcharaza viboko na kumtusi. Wakati mwanaume huyo alikuwa akijaribu kupata fahamu na kujiokoa, Dorothy alianza kuitisha usaidizi kwa majirani.

Alipofika nje, majirani tayari walikuwa wamejaa, akiwemo mkewe ambaye vilevile alikuwa amefika kushuhudia.

Mara hiyo hiyo, mwanamke huyo mpango wa kando wa Mwata anasemekana kuchana mbuga kujiokoa kutoka kwa mkewe ambaye alikuwa akitaka kumvamia na hajaonekana tena. Mkewe Mwata naye vilevile aliondoka nyumbani kwake pamoja na wanawe wawili wa miaka 11 na 16 na kuapa kuwa hatarudi.

Mwata pia, ambaye ni mfanyakazi wa umma ameripotiwa kutoroka mjini humo, kwani hadi sasa hajaonekana tena.