Makala

Kioja cha ukahaba kuvuma makanisani

March 23rd, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Uthiru, ni mojawapo ya mitaa inayounda kaunti ya Kiambu, na ambao ramani inaonyesha unapatikana katika eneobunge la Kabete.

Mtaa huo u kati ya Kikuyu na Kangemi, takriban kilomita 18.3 kutoka kitovu cha jiji la Nairobi.

Sawa na mitaa mingine Nairobi na Kiambu, wakazi na wenyeji wa Uthiru wanaendesha shughuli mbalimbali angalau kukithi mahitaji yao ya kimsingi na kujiendeleza kimaisha.

Katika mtaa huohuo, kinapatikana kitongoji cha Mariguini, ambacho sawa na jina lake lenye asili ya Agikuyu linalomaanisha ‘ndizi’ kimesheheni migomba inayozalisha matunda hayo.

Upande mmoja wa Mariguini umepakana na barabara kuu inayounganisha Nakuru, Naivasha na jiji la Nairobi.

Unapoabiri gari Nairobi kuelekea kitongoji hicho, kabla kutua utapitia ‘Uhuru Park’ ndogo, bustani ambayo wikendi huwa na shughuli kibao hasa za kuburudisha na kufurahisha watoto.

Barabara ya lami inayoelekea Mariguini kutoka barabara kuu ya Nairobi – Naivasha – Nakuru. Picha/ Sammy Waweru

Kando na kulakiwa na migomba, baadhi ya wenyeji hususan wenye ploti na mashamba wameingilia shughuli za kilimo, ingawa kwenye viunga na vivungulio – mahema.

Kuna wanaokuza karoti, spinachi, sukuma wiki, kabichi, na mboga zingine asilia, pamoja na mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha na kuvuna.

Ipatayo miaka mitatu iliyopita, Wanjiru Kagotho alihamia Mariguini, baada ya kupata nafasi ya kazi katika mojawapo ya afisi za shirika la Price Water House Coopers, ndiyo PWC, Westlands, kama mpishi na mhudumu.

Hiyo ilikuwa baada ya kufanya vibarua vya hapa na pale eneo la Ruai, Nairobi, na alipopata fursa hiyo hakusita kuikumbatia.

Mtaa ulio karibu na uliomfurahisha kuishi ili kupunguza gharama ya usafiri ukawa Uthiru. Wanjiru anasema alielekezwa kutafuta nyumba ya kukodi ya bei nafuu katika kitongoji cha mabanda cha Mariguini.

Wanjiru Kagotho, anaishi eneo jirani na Mariguini. Alionywa dhidi ya kuishi humo kwa sababu ya utovu wa usalama. Picha/ Sammy Waweru

Hilo kwake lilikuwa pendekezo bora, akitumai ataweza kulea familia yake changa. Alitenga siku, akajituma kutafuta nyumba, na ni katika harakati hizo alikutana na mama mkongwe aliyemtahadharisha dhidi ya kuishi humo.

“Baada ya kunikagua kwa macho kwa muda, aliniambia hadhi yangu hainiruhusu kuishi katika nyumba za mabanda za Mariguini. Hakunieleza bayana sababu za kunionya,” Wanjiru ambaye ni mama wa watoto wanne anakumbuka.

Isemwavyo wazee waliokula chumvi wana maneno ya busara, hakuwa na budi ila kutii ushauri wa mama huyo, anayemtaja kama ‘muungwana na msamaria mwema’.

Alipata nyumba anayomudu kulipa kodi katika kitongoji jirani na Mariguini, hiyo ikiwa na maana kuwa akielekea kazini na kurejea hupitia pembezoni mwa alikoonywa kutoishi.

Mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu na miezi kadhaa ikayoyoma akiendelea kugubikwa na maswali “kwa nini huyo mama alinionya kuishi mabanda ya Mariguini, ilhali huskia yana nyumba za bei nafuu?”

Mwaka wa kwanza ulipokamilika, alianza kupevuka, akafumbuka macho na akili. Wanjiru anasema mwaka wa pili alikuwa na taswira kamili ya filamu ya Mariguini.

Mtaa wa mabanda aliotamani kwa sifa za kodi nafuu ya nyumba, una hulka za kipekee. “Mariguini ina zaidi ya makanisa 20 ambayo kila Jumapili mchana anga yake huhinikiza mahubiri na nyimbo za kumtukukuza, kumshukuru na kuabudu Mwenyezi Mungu.

“Kuanzia jioni, usiku kucha hadi asubuhi, mambo huwa tofauti kabisa na yanayofanyika mchana kutwa,” Wanjiru akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano katika eneo hilo.

Wanjiru Kagotho, anaishi eneo jirani na Mariguini. Alionywa dhidi ya kuishi humo kwa sababu ya utovu wa usalama. Picha/ Sammy Waweru

Hadithi ya Sodoma na Gomora, huisoma kwenye Biblia na vitabu vya historia vya kidini, na kulingana na mkazi huyo sifa za Mariguini zinawiana na hadithi hiyo.

Licha ya eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya makanisa, Wanjiru anasema ukahaba na uzinzi ndio ratiba ya kitongoji hicho kuanzia majira ya jioni, usiku hadi kunapokucha, kila siku.

“Kwa kuwa ninahudumu katika mkahawa, ninaporatibiwa kuhudumu usiku, ninapoelekea kazini jioni hujionea makuu ‘watu wakiingia kazini Mariguini na wakitoka asubuhi’ ninaporejea,” afafanua.

Isitoshe, ni katika mazingira yayo hayo yenye makanisa Wanjiru anasema mihadarati na dawa za kulevya hulanguliwa na kuuzwa.

Job Njuguna ambaye pia ni mkazi anafichua kwamba uuzaji wa pombe haramu Mariguini si jambo geni, na hufanyika mchana peupe.

“Pombe haramu kama vile chang’aa eneo hili la Uthiru hupatikana kwa urahisi hapa Mariguini,” Njuguna anaeleza.

Ni katika mazingira yayo hayo, tawi la kanisa la Nabii maarufu Dkt Edward David Awuor lipo.

Visa hivyo vikijumuishwa, kiwango cha usalama ni wazi kimedorora. “Changamoto kuu Mariguini ni utovu wa usalama, watu hulaghaiwa na kuibwa mali yao mchana. Usiku hakipitiki,” kauli ya pamoja iliyoradidiwa na wakazi tuliozungumza nao.

Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza majeraha, unapozuru Mariguini majira ya asubuhi hutakosa kutazama vijana na hata wazee wakitoka kwenye mabanda wakiwa walevi chakari.