Habari Mseto

Kioja maafisa wa kaunti kufukua maiti na kuivua sare za kazi

August 14th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

WAKAZI wa kijiji cha Eburinde, Butere, Kaunti ya Kakamega waliachwa vinywa wazi Jumanne baada ya maafisa wa serikali ya kaunti kufukua maiti ya mwenzao aliyezikwa na sare za kazi.

Martin Shikuku Alukoye, 31, aliyekuwa akifanya kazi katika idara ya Huduma ya Vijana katika Kaunti ya Kakamega, alikufa maji baada ya kutumbukia ndani ya Mto Eburinde Agosti 7.

Alizikwa usiku wa kuamkia Agosti 11, kwa mujibu wa mila na desturi za jamii ya Waluhya kuhusiana na mtu anayekufa maji.

Inasadikiwa kuwa mwendazake alikuwa akiugua maradhi ya kifafa na alizimia alipokuwa akivuka mto.

Alizikwa akiwa amevalia sare za idara ya huduma ya vijana, ikiwemo kofia, viatu na kitambulisho cha kazi.

Mnamo Agosti 12, msimamizi wa eneo la Ituti akiwa na ameandamana na maafisa wengine wa kaunti, walizuru nyumbani kwa mwendazake kuchukua sare lakini wakafahamishwa kwamba alizikwa na kila kitu.

Maafisa hao walisisitiza kufukua maiti ili watoe sare za kaunti.

Juhudi za familia kuwataka maafisa hao wa kaunti waache kufukua kaburi la mwanao ziliambulia patupu.

Maafisa wa kaunti bila kuwa na kibali kutoka kortini walifukua maiti ya mwendazake kwa nguvu.