Kioja mama akiuza shamba aponde raha

Kioja mama akiuza shamba aponde raha

Na JOHN MUSYOKI

KIVAA, MASINGA

WAKAZI walishuhudia sinema ya bwerere mwanamke mmoja alipoamuru nyumba ya mwanawe ibomolewe ili auze shamba alikoijenga.

Siku ya kisanga mke wa jamaa alipokuwa akifanya shughuli zake nyumbani, alipigwa na mshangao, mama wa mumewe alipokita kambi kwake na watu wasiojulikana.

Alianza kumgombeza mkaza mwanae akimtaka aondoke katika shamba lake.

“Wewe na mwanangu nataka mtoke kwa shamba langu. Chukua kilicho ndani nataka kuuza shamba hili la marehemu mume wangu,” mama alisema.

Maneno ya mwanamke huyo yalishangaza.

Watu walianza kunong’onezana huku na kule huku kila mmoja akitoa kauli yake kuhusu alichodhani kilipelekea mwanamke huyo kuamua kumfurusha mwanawe na mke wake.

“Mwanamke huyu ni kisirani sana. Hata kabla ya mumewe kuaga dunia alikuwa akidai kuishi maisha ya raha mstarehe lakini mumewe wakati huo hakumpa nafasi ya kumkalia chapati,” mmoja wa majirani wa mama huyo alisema.

Naye mwanamke mwingine alinukuu maneno ya mwanamke huyo kabla ya kifo cha mumewe, akidai alisema kuwa: “Mume wangu amekuwa akininyima raha kwa muda mrefu. Akitoka katika dunia hii nitatawala na kuishi maisha ya raha. Nitakuwa ninakula chakula nikipendacho kila siku. Shamba nitauza na mifugo pia na mwanangu akileta pang’ang’a nitamfunza adabu.”

Bila kujali watu waliokusanyika, mwanamke huyo aliamuru nyumba ya mwanawe ibomolewe.

Aliuza shamba hilo na ikabidi mke wa mwanawe kwenda kwa wazazi wake kwa kuwa wakati wa kisanga hicho mumewe hakuwa karibu.

Wakazi walikashfu kitendo cha mwanamke huyo ila hakuna aliyethubutu kuingilia kati kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa moto wa kuotea mbali.

“Tamaa ya pesa itampeleka mwanamke huyu wapi? Sasa ameuza shamba mpaka kaburi la mumewe ili aponde raha mwanawe akiteseka,” mwanakijiji mmoja alilalamika.

Hata hivyo haikujulikana mwana wa mwanamke huyo alichukua hatua gani baada ya mamake kubomoa nyumba yake na kuuza shamba.

You can share this post!

Mabadiliko yafanyika katika ngazi za utawala maeneo kadha...

Jumwa adai serikali ya Kingi haijali wakazi