Habari

Kioja miili ya mwanamume na mwanamke kupatikana na kondomu ndani ya kanisa

July 16th, 2018 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Kirinyaga wanachunguza kisa ambapo miili ya mwanamume na mwanamke iliyokuwa uchi wa wanyama na kondomu kando ilipatikana ndani ya kanisa moja Jumamosi.

Miili hiyo ilipatikana katika kanisa la Holy Ghost Terbancle eneo la Muringe, kaunti ndogo ya Ndia.

Kando ya miili hiyo kulikuwa na mipira miwili ya kondomu iliyokuwa imetumika.

Hapo Jumapili, waumini wa kanisa hilo waliabudu nje huku kiongozi wake Askofi Kinyua Nyaga akisema leo kutakuwa na hafla ya utakaso wa kanisa hilo ambapo maaskofu wengine wataongoza harakati hizo.

Askofu Nyaga alisema atangojea uchunguzi wa polisi ili apate jibu kuhusu kisa hicho, au asubiri Mungu ampe ufunuo wa kile hasa kilifanya kanisa lake kupatwa na kisa hicho.

Tukio hilo lilizua mjadala miongoni mwa wenyeji, baadhi wakisema kuwa hiyo ilikuwa “adhabu ya Mungu kwa wawili hao kuzini ndani ya kanisa”.

Hata hivyo haijabainika iwapo walikuwa wakizini ama waliuawa na miili kutupwa humo kanisani, na ni masuala haya ambayo polisi wanachunguza

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Polisi wa Utawala wa eneo hilo, Boniface Mwaniki, wenda zao walikuwa wameonekana awali katika mji wa Kagio wakinywa pombe pamoja, na walitoka baa walimokuwa mwendo wa saa nne usiku.

“Habari tulizo nazo kwa sasa ni kuwa wawili hao, ambao hakuna anayewafahamu eneo hili, walikuwa wameingia katika baa hiyo mwendo wa saa mbili jioni na wakaanza kulewa. Imebainika kuwa mwanamke huyo, ambaye anakadiriwa kuwa wa miaka ya 40, ndiye aliyekuwa akilipa bilizake na za kijana anayeonekana kuwa wa miaka 30 hivi,” akasema Bw Mwaniki.

Alieleza kuwa taarifa za mashahidi waliowaona wawili hao wakitoka baa hiyo zinaonyesha kuwa walitembea kuelekea barabara ya Makutano – Sagana.

“Kile ambacho kimebakia kuwa kitendawili ni jinsi wawili hao waliishia hapa kanisani, ilikuwaje wakawa uchi, nguo zao zilikuwa kando mwa miili yao, kuna kondomu zilizotumika na walikumbana na mauti vipi. Wote wawili hawana majeraha ya kuashiria walishambuliwa na walikuwa wamelala wakiwa wamekaribiana na nyuso zao zikiwa sambamba,” akasema afisa huyo.

Bw Mwaniki alisema kisa hicho kinachunguzwa na maafisa wa DCI eneo hilo ili kujaribu kutegua kitendawili hicho.

Alisema kuwa kanisa hilo ambalo limejengwa kwa mbao na mabati lilikuwa limevunjwa kufuri ya mlango.

“Nje ya kanisa hilo kuna alama za magurudumu ya pikipiki. Licha ya mmiliki wa baa walimokuwa wakibugia pombe kusema kuwa alikuwa amewapa wawili hao chenji ya Sh450 walipokuwa wakitoka, hakuna pesa zilizokuwa katika eneo hilo la mauti,” akasema Bw Mwaniki.

Alieleza kuwa miili hiyo ilipelekwa katika mochari ya Embu kuhifadhiwa huku uchunguzi zaidi ukiendelezwa.

“Kwa sasa, tumechukua alama za vidole za miili hiyo na pia mipira ya kondomu ili kuchunguza kama uchafu ulio ndani yazo ni wa ngono ya wawili hao au ni wa mwingine,” akasema.

Alisema kuwa uchunguzi zaidi utatekelezwa katika upasuaji wa miili ili kufahamu jinsi walivyoaga.