Dondoo

Kioja mke kutoa gari la mzee sadaka

February 1st, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MALAA, Machakos

KULITOKEA kizaazaa mtaani hapa buda mmoja alipotisha kuwaita polisi kumkamata mkewe na pasta wake akidai walikuwa wameshirikiana kuiba gari lake.

Kulingana na mdaku wetu, buda alikuwa amesafiri nje ya nchi kwa shughuli za kikazi na kuacha mkewe kuchunga mali yake likiwemo gari la kifahari.

Inasemekana kuwa mkewe ambaye ni mshirika wa kanisa moja mtaani hapa alivutiwa na jinsi watu walikuwa wakipokea miujiza wakitoa sadaka nono. Pasta wa kanisa hilo, alikuwa akiwashawishi washirika kutoa kwa ukarimu ili wabarikiwe zaidi.

“Kadri unavyotoa sadaka nono kwa ukarimu ndivyo Mungu anakubariki, mkitoa chochote unapokea maradufu,” pasta alikuwa akiwaeleza washiriki.

La kushangaza ni kuwa, mke wa buda hakufahamu kuwa pasta huyo alikuwa tapeli aliyekuwa akibuni miujiza ili kuwavutia washirika zaidi katika kanisa lake.

Kwa mujibu wa mdokezi, pasta huyo alikuwa akiwalipa watu ili watoe ushuhuda wa uwongo kwamba walikuwa wamepokea miujiza baada ya kuombewa na kutoa sadaka nono.

Yasemekana mama huyo aliamua kupeana gari la mumewe kwa matarajio ya kupokea nyingine kwani aliambiwa baada ya wiki tatu angekuwa amepokea magari mawili kama hayo.

Kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa anafahamu mumewe angewasili baada ya mwezi mmoja, alitarajia kupata muujiza kabla ya mumewe kuwasili lakini haikuwa hivyo kwani aliwasili kabla ya unabii wa pasta kutimia.

Yasemekana buda alipokosa gari lake alizusha akitaka kujua lilikuwa wapi.

“Alimchemkia mkewe na ikabidi amweleze ukweli. Buda alikasirika na kutisha kuwaita polisi kumkamata mkewe na pasta wake iwapo hangepata gari lake kwa muda nusu saa,” alisema mdokezi. Ilibidi mwanadada kwenda kwa pasta kuchukua gari hilo kujinusuru.