Dondoo

Kioja polo akidai kufufua maiti

February 5th, 2020 1 min read

Na Tobbie Wekesa

SINOKO, BUNGOMA

KIOJA kilizuka katika mazishi eneo hili baada ya polo kudai ana uwezo wa kumfufua marehemu.

Inasemekana polo alipowasili mazishini, alikuta jamaa wa mwendazake akisoma wasifu wa marehemu.

Duru zinasema kalameni alienda moja kwa moja hadi kwenye jeneza na kuutazama mwili kwa takriban dakika kumi. Kisha akaelekea hadi walikokuwa wameketi waombolezaji wengine.

Wakati wa pasta kutoa mahubiri ulipowadia, mwanamume huyo aliinuka kwa haraka na kuomba apewe kipaza sauti.

“Nipeni maikrofoni. Huyu jamaa aliyelala hapa hajafa. Nina uwezo wa kumuamsha kutoka usingizini,” alisema kwa sauti ya juu.

Kila mmoja aliinuka amuone polo. “Mungu amenituma hapa kumfufua mwenzetu,” alieleza. Pasta alimpuuza na kuendelea na mahubiri.

“Huyu jamaa ni bangi inamsumbua. Pia ni mkora sana. Pasta endelea na ibada,” mmoja wa waombolezaji alisikika akisema.

Inadaiwa kalameni aliendelea kudai apewe nafasi. “Nimefufua wengi sana. Huyu kwangu ni kazi kidogo. Sitaki mnilipe chochote. Nikishamfufua atanilipa!” Akasababisha vicheko kusikika mazishini. Hata waliokuwa wakitoa machozi kutokana na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao walibaki vinywa wazi.

“Hata mimi mwenyewe nilikuwa nimekufa wakati fulani lakini nikafufuka. Nikimaliza shughuli yangu mtaendelea na ibada yenu,” polo aliwarai waombolezaji. Habari zilizotufikia zinasema kuwa, waombolezaji hao waliamua kumtimua huku wakimsisitizia pasta aendelee na mahubiri.

“Mchungaji, huyu mtu anasumbuliwa na pepo. Aondoke hapa haraka. Hana uwezo wowote,” jamaa wa marehemu walifoka.

Kalameni alilazimika kuchomoka mbio huku vijana wakimfuata kumuadhibu.