Dondoo

Kioja polo kulilia nje ya lango la lojing'i

February 13th, 2019 1 min read

Na Nicholas Cheruiyot

Kericho Mjini

Kulikuwa na tukio la kipekee katika lojing’i moja mjini hapa, polo alipodai kwamba alisahau kipochi ndani ya chumba baada ya kumaliza kurushana roho na kimada mmoja.

Inaarifiwa kuwa gesti hiyo hupendwa sana na makalameni wanaofanikiwa kupata windo mchana peupe.

Siku ya tukio, polo alifika gesti na kichuna na baada ya dakika chache shughuli ilikuwa imeisha na wakatoka kwenda zao.

Baada ya muda wa saa moja, polo alirudi akihema na kulia kwamba alikuwa ameacha kipochi kilichokuwa na hela zote ndani ya chumba.

Shida ilitokea kwani tayari chumba hicho tayari kilikuwa kimepata wateja wengine waliokuwa wametawaliwa na tamaa ya kula uroda mchana kama yeye.

Wahudumu walidinda kumsaidia polo wakiteta hawakutaka kuharibia wateja raha zao. “Wateja wengine washaingia huko na hatutawasumbua wakiponda raha. Subiri hadi watoke kwa hiari yao,” mhudumu mmoja alimwambia polo.

Hata hivyo, jamaa hakuridhika hata kidogo.

“Polo alienda na kupiga mlango uliokomolewa ndani akiomba afunguliwe atoe kipochi lakini jamaa aliyekuwa ndani alinguruma tu kwa hasira kisha akaendelea na shughuli yake. Sinema ya bure ilitokea polo akililia kipochi na waliokuwa ndani walisikika wakitikisa kitanda wakishiriki tendo,” mdaku alieleza.

Hatimaye, waliokuwa ndani walikata kiu na wakatoka nje. Polo naye alijitoma ndani na kubahatika kupata kipochi chini ya kitanda.

“Sioni nikija tena hapa kula uroda kwani nusura nipoteze donge baada ya kupandishwa mzuka na kidosho huyo,” polo aliambia wahudumu tabasamu likimejaa usoni kwa kupata kipochi kisha akawataja wafanyikazi wa huko kama wachoyo kwa kutomsaidia.

Kabla ya kuondoka, wahudumu walimshauri asiwatusi wakunga maana uzazi bado ungalipo.