Kimataifa

Kioja wanaume kwenda haja kubwa ufuoni mbele ya watoto

January 14th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

FAMILIA zilizokuwa zinajiburudisha kwa muziki katika ufuo wa bahari nchini Australia ziliachwa katika mshangao mkubwa, baada ya wanaume wawili kuvua nguo zote, na wakiwa uchi wa mnyama kuanza kwenda haja kubwa baharini.

Wakazi walikuwa wakijiburudisha katika ufuo wa Lamberts, kaskazini mwa eneo la Queensland Jumamosi walipokumbwa na tukio hilo la kushangaza.

Shahidi kwa jina Lance Payne alisema kuwa aliwatazama wanaume hao tangu walipotoka kutoka gari lao ufuoni na kuanza kuvua mavazi, huku wakikimbia kwa kuzunguka ufuo.

Bw Payne alisema kuwa mmoja wa wanaume hao alianza kukojoa katika bahari, kisha mwenzake akajiunga, na baadaye wakaanza kwenda haja kubwa.

“Alitembea hadi kwenye maji, akavua suruali na kuinama kwa kukunja magoti kisha akakaa hivyo,” shahidi huyo akaeleza shirika moja la habari.

Umma ulivutwa na vitendo vyao wakati mmoja wa wanaume hao alionekana kujikaza na kuhema, ndipo wakabaini alikuwa akienda haja kubwa majini.

Shahidi huyo aliripoti kisa hicho kwa polisi baadaye, akisema kuwa kutokana na namna walivyotembea, walionekana kama waliokuwa wametumia dawa za kulevya.

Ilisemekana kuwa kulikuwa na watoto wengi ufuoni ambao huenda waliadhirika na tabia hiyo chafu ya wanaume hao.

Hata hivyo, polisi hawakuweza kuwakamata wanaume hao kwani walisema ripoti ilipigwa ikiwa imechelewa, na kuwa ushahidi kuhusu sura zao haukutosha.