Habari Mseto

Kioja waombolezaji wakiachiwa mwili Likoni

April 29th, 2019 1 min read

Na HAMISI NGOWA

KULITOKEA kioja katika eneo la Likoni mwishoni mwa wiki, familia moja iliyokuwa ikisafirisha maiti ya jamaa wao ilipoachiwa mwili na dereva wa matatu.

Kizaazaa kilianza ndani ya feri ya Mv Jambo pale dereva wa matatu iliyokuwa imeubeba mwili wa marehemu alipokataa ombi la jamaa za marehemu kumtaka asimamishe gari eneo la Klabu ya The Ofice ili kutoa nafasi kwa baadhi ya marafiki za marehemu kutoa heshima zao za mwisho.

Malumbano baina ya dereva wa matatu na jamaa za marehemu yalivutia umati wa abiria waliokuwa kwenye feri hiyo na kuwalazimu waingilie kati ili kutuliza hali baada ya joto kuzidi.

Hata hivyo, kivumbi kilishuhudiwa karibu na Benki ya Rafiki matatu hiyo ilipoenda kuegeshwa ili kuwasubiri waombolezaji wakati magari yaliporuhusiwa kutoka kwenye feri hiyo.

Familia ya marehemu ikiongozwa na kakayake mdogo Simon Joseph na dadake Bi Patrecia Joseph walisisitiza kwamba lazima maiti ya marehemu ishukishwe ili kuwapa nafasi waliokuwa marafiki zake pamoja na wafanyabiashara wenzake kuutazama mwili kwa mara ya mwisho.

Tukio hilo lilizua hali ya mshike mshike na kufanya afisa wa polisi wa utawala aliyekuwa akishika doria nje ya Benki hiyo kuwafurusha.

Baada ya tukio hilo, dereva wa matatu hiyo alielekea hadi eneo la Klabu ya The Ofice ambako aliamua kuushukisha mwili wa marehemu kutoka kwenye gari hilo na kisha kuwababeba baadhi ya waombolezaji na kuelekea kijiji cha Magangani Vanga Lunga Lunga ambako mwili huo ulitarajiwa kupelekwa.

Dereva huyo wa matatu inayohudumu baina ya Lunga Lunga na Likoni ambaye alikataa kutambuliwa kwa jina, alisema hafai kulaumiwa kwa tukio hilo kwani hakuwa amelipwa kubeba maiti.

“Mimi nilikuwa nimelipwa kubeba waombolezaji kutoka hifadhi ya maiti ya Hospitali kuu ya Rufaa mjini Mombasa hadi Magangani lakini nilipoona gari linalobeba maiti ni dogo nikaamua kuibeba juu ya keria ya gari langu,” akasema.