Kioja waumini wakivunja makufuli sita kanisani

Kioja waumini wakivunja makufuli sita kanisani

Na RUSHDIE OUDIA

KISANGA kilizuka Jumapili asubuhi katika kanisa moja mjini Yala, Kaunti ya Siaya, baada ya kundi la waumini waliojawa na ghadhabu kuvunja kufuli ili waweze kuingia katika nyumba ya Mungu.

Kanisa hilo lilidaiwa kufungwa na viongozi wa kidini wiki mbili zilizopita kufuatia mzozo kuhusu uongozi. Katika mkondo usiotarajiwa, kufikia saa kumi na mbili unusu asubuhi, waumini walikuwa wamekusanyika nje ya kanisa hilo wakiwa na silaha mbalimbali zikiwemo msumeno na vyuma ambavyo kwa kawaida hutumiwa kuchimba mawe, wakiwa tayari kuingia ndani ya kanisa hilo kwa nguvu.

Kufikia saa mbili asubuhi, walikuwa wamevunja kufuli lililokuwa kwenye lango, kisha wakang’oa makufuli matatu yaliyokuwa kwenye lango kuu la kanisa hilo na baadaye wakavunja makufuli mengine mawili ili waweze kuingia.

Huku wakiendelea na shughuli za kuvunja makufuli hayo, waimbaji wa kwaya walikuwa wakiimba nyimbo za kuvutia wakiwashangilia na walipoingia hatimaye, wakapangusa viti, wakafungua madirisha na kuendelea na ibada kama kawaida huku watu wengine wakizidi kufurika ndani ya kanisa hilo.

Kulingana Naibu Mwenyekiti wa kundi la waumini wa kawaida wasio viongozi, Bw Odongo Onyango, waumini wamepokonywa kanisa hilo kinyume na utaratibu unaofaa.

Bw Onyango alimshutumu Mzee wa Kanisa hilo, Edward Otieno Onyango na Mwinjilisti Judith Magudha dhidi ya kuwafungia nje ya kanisa mnamo Januari 5.

Kisha mnamo Januari 12, wakiwa na kibali kutoka kwa Askofu wa Dayosisi hiyo, viongozi wa kanisa hilo waliongeza kufuli jingine kwa waliyokuwa wameweka awali na kuwafungia kabisa Wakristo hao nje ya kanisa, jinsi walivyokiri mbele ya Kamanda wa Polisi katika Kituo cha Polisi cha Yala.

“Hatujui ni kwa nini kwa sababu hatukushirikishwa na kulingana na katiba kanisa ni la waumini,” alisema Bw Onyango.

Alisema kwamba kutokana na uamuzi huo, Askofu wa Dayosisi hiyo na kundi lake wamekiuka haki zao na uhuru wa kikatiba wa kukusanyika na kuabudu.

Na baada ya kukaa wiki mbili nyikani, Wakristo hao waliamua kuchukua sheria mikononi mwao na kuwanyorosha wale wanaowashutumu dhidi ya kukiuka haki zao kwa kuwanyima fursa ya kufanya ibada.

You can share this post!

Boca Juniors wanyanyua taji la kwanza la Diego Maradona Cup

Ulinzi mkali mmoja akinaswa akiwa na bastola, risasi 500...