Michezo

Kioko atajwa kocha mpya wa makipa wa Mathare

July 10th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Mathare United imemteua aliyekuwa mchezaji wa Zoo Kericho FC Samuel Kioko kama kocha mpya wa makipa wake.

Kioko ambaye awali alishikilia wadhifa uo huo akiwa Zoo, ataleta tajriba pana kwenye idara hiyo ambayo kuvuja kwake kulikuwa dhahiri kama meno ya ngiri wakati wa kichapo walicholishwa cha 3-2 mikoni mwa Sofapaka kwenye mechi ya  Jumapili Tarehe 8 mwaka 2018.

Mkufunzi huyo ambaye pia alichezea Nairobi Stima atakuwa na jukumu kubwa la kutia makali mnyakaji wa Mathare United David Okello aliyefanya masihara mengi langoni wakati wa mchuano huo na kuwazawidi ‘Batoto ba Mungu’ bao la kwanza.

“Kioko analeta mwamko mpya katika kitengo chetu cha makipa haswa baada ya kufanya kazi kwa karibu na aliyekuwa kipa matata wa Harambee Stars Willis Ochieng’ kama mkufunzi wake akiwa Zoo FC, “ ikasema taarifa kutoka mtandao wa Mathare United.

‘Vijana wa mtaa wa mabanda’ wanashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa jedwali la ligi kwa alama 34 huku wakitarajiwa kuvaana na limbukeni Wazito FC kwenye uwanja wa Kenyatta mjini Machakos Jumamosi 14 mwaka 2018.

Mathare United hawajaweza kutwaa ushindi katika mechi zao saba zilizopita.