Michezo

Kiongera aahidi makuu kambini mwa Sofapaka

September 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO 

FOWADI wa zamani wa Harambee Stars, Paul ‘Modo’ Kiongera, amejiwekea malengo ya kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya kuingia katika sajili rasmi ya Sofapaka.

Kiongera aliyenyanyua taji la KPL akichezea Gor Mahia, amewataka mashabiki na wakosoaji wake kukoma kumwita “mkongwe” na kutarajia makuu kutoka kwake kambini mwa Batoto ba Mungu wlaiotawazwa wafalme wa KPL kwa mara ya mwisho mnamo 2009.

“Tuna furaha kufichua kwamba tumemsajili Kiongera ambaye atakuwa mwanasoka wetu kwa kipindi cha misimu miwili ijayo,” ikasema sehemu ya taarifa ya Sofapaka.

Hadi kujiunga kwake na Sofapaka baada ya kuagana na Wazito FC, Kiongera aliwahi pia kucheza Gor Mahia, AFC Leaopards, KCB na Simba SC ya Tanzania.

Makali ya Kiongera ambaye alifahamika kwa kasi na wepesi wa kutikisa nyavu za wapinzani miaka sita iliyopita, yalishuka sana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na akateremka hadi kushiriki soka ya Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

 “Kubwa zaidi katika malengo kwa sasa ni kuendelea kufunga mabao katika KPL ndani ya jezi za waajiri wangu wapya,” akatanguliza Kiongera.

“Tuna kocha mzuri, John Baraza, ambaye anaelewa kinachohitajiwa na mshambuliaji yeyote na aina ya wachezaji watakaomwezesha kufikia mengi ya maazimio yake. Nina imani kwamba nitafurahia maisha yangu Sofapaka na kwamba kikosi hiki kitachangia ufufuo wa makali yangu ya awali,” akaongeza mvamizi huyo.

Chini ta Rais Elly Kalekwa, Sofapaka wana kiu ya kutwaa ubingwa wa KPL kwa mara ya kwanza baada ya kunyanyua taji hilo miaka 11 iliyopita katika msimu wao wa kwanza ligini.

Mbali na Kiongera, Sofapaka wamejinasia pia huduma za wanasoka Wisdom Maya na Joel Nokueou kutoka kambini mwa Lion Blesse nchini Ghana.

Kiongera na kiungo Lloyd Wahome ndio wanasoka wa hivi karibuni zaidi kubanduka kambini mwa Wazito ambao wametema jumla ya wanasoka 14.

Wahome alijiunga na Wazito mnamo mnamo Machi 2019 baada ya kuvunja ndoa yake ya miaka mitano na mabingwa mara 11 wa KPL, Tusker FC.

Kiongera alisajiliwa na Wazito kwa mkataba mfupi mnamo Januari 2020.

Paul Acquah (Ghana), Issifou Bourahana (Togo), Augustine Out (Liberia) na Piscas Kirenge (DR Congo) ni wanasoka raia wa kigeni ambao walikuwa miongoni mwa 12 waliotimuliwa na Wazito FC mwezi uliopita.

Wachezaji wa humu nchini ambao pia wamebanduliwa kutoka kikosi cha Wazito ni aliyekuwa fowadi wa SoNy Sugar Derrick Otanga, kipa mzoefu Steven Njung’e, kiungo Teddy Osok, mshambuliaji wa zamani wa Tusker Victor Ndinya na kipa chaguo la kwanza katika kampeni za msimu jana, Kevin Omondi aliyewahi pia kuvalia jezi za SoNy Sugar.