Kiongozi wa IS auawa nchini Somalia

Kiongozi wa IS auawa nchini Somalia

NA AFP

WASHINGTON, Amerika

KIONGOZI wa kundi la kigaidi la Islamic State (IS), Bilal al-Sudani, ameuawa katika shambulio lililotekelezwa na wanajeshi wa Amerika nchini Somalia, kufuatia agizo la Rais Joe Biden.

Sudani aliuawa juzi wakati wa makabiliano ya risasi jioni baada ya wanajeshi wa Amerika kuvamia pango moja kwenye eneo la milima kaskazini mwa Somalia wakilenga kumkamata, kulingana na maafisa wa Amerika.

Washirika 10 wa kundi hilo la Sudani waliokuwa eneo hilo waliuawa, lakini hakuna mwanajeshi wa Amerika aliyekufa, maafisa hao wakaongeza.

“Mnamo Januari 26 kufuatia amri ya Rais, wanajeshi wa Amerika waliendesha operesheni kaskazini mwa Somalia iliyosababisha kuuawa kwa wafuasi kadha wa IS, akiwemo Bilal al-Sudani,” Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin akasema kwenye taarifa.

“Al-Sudani alihusika katika kuendeleza uwepo wa wapiganaji wa IS Afrika na kwa kufadhili operesheni za kundi hilo kote ulimwenguni, ikiwemo nchini Afghanistan,” Austin akasema.

Kutoka ngome yake eneo la milimani kaskazini mwa Somalia, alitoa na kushirikisha ufadhili kwa matawi ya IS, sio tu Afrika bali barani Afrika lakini pia kwa kundi la Islamic-State Khorasan, kundi linalofanya mashambulio nchini Afghanistan, akasema afisa wa Amerika aliyeomba jina lake libanwe.

Miaka kumi iliyopita, kabla yake kujiunga na kundi la Islamic State, Sudani alihusika katika usajili na utoaji mafunzo kwa wapiganaji waliosajiliwa katika kundi la Al-Shabaab nchini Somalia.

“Sudani alikuwa na wajibu mkubwa kioperesheni, kifedha na kiujuzi hali iliyomfanya kulengwa zaidi katika mpango wa Amerika wa kupambana na ugaidi,” afisa huyo alieleza.

Operesheni ya Alhamisi ilikuwa imepangwa kwa miezi kadha, huku wanajeshi wa Amerika wakifanya mazoezi katika eneo lililowakilisha mandhari ambako Sudani alikuwa amejificha.

Rais Biden aliamuru shambulio hilo mapema wiki hii baada ya kufanya mashauri na maafisa wakuu wa jeshi, idara za ujasusi na usalama.

“Hatimaye operesheni ya kumkamata iliamuliwa kuwa njia bora ili kuimarisha ufanisi wake katika mandhari hiyo yenye changamoto,” afisa mwingine wa Amerika akasema.

Hata hivyo, hatua ya washirika wa Sudani kujibu shambulio la wanajeshi wa Amerika ndio ilichangia kifo chake.

Ni mwanajeshi mmoja wa Amerika wa cheo cha chini ndiye aliyejeruhiwa baada ya kuumwa na mbwa wa kijeshi, afisa huyo akaongeza.

Mwaka 2022, Rais Biden alitangaza kujitolea kwa serikali yake kumaliza kabisa vitisho vya ugaidi. dhidi ya Amerika na watu wake. Aliahidi kuwaandama magaidi “popote walipojificha, misituni, milima na mabonde.”

Wanajeshi wa Amerika wameendesha operesheni dhidi ya magaidi nchini Amerika kwa muda mrefu, kwa ushirikiano na au kwa niaba ya serikali ya Somalia.

Aidha, wanajeshi wa Amerika wametekeleza mashambulio ya kila mara ya angani kupiga jeki wanajeshi wanaopambana na Al-Shabaab nchini Somalia.

  • Tags

You can share this post!

Wavuvi Kilifi watakiwa wawe waangalifu upepo mkali ukivuma...

Hakukuwa na wizi wa KCSE, Machogu ajibu

T L