Kiongozi wa upinzani nchini Zambia akaribia kuwa Rais

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia akaribia kuwa Rais

Na MASHIRIKA

LUSAKA, ZAMBIA

KIONGOZI wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema, Jumamosi aliandikisha uongozi wa mapema dhidi ya rais wa sasa Edgar Lungu, kulingana na matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi.

Hichilema alikuwa kifua mbele baada ya kuzoa jumla ya kura 171,604 kulingana na matokeo yaliyotangazwa kutoka maeneo bunge 15 kati ya maeneo bunge 156 nchini humo.

Rais Lungu alikuwa anamfuata kwa kupata jumla ya kura 110,178 katika maeneobunge hayo.

Maeneo hayo yanachukuliwa kuwa ngome ya Rais Lungu, hali ambayo wadadisi wanasema inaashiria kuwa Hichilema ataibuka mshindi katika uchaguzi wa mwaka huu wa urais.

Upigaji kura ulifanyika Alhamisi na kulingana na katiba ya Zambia matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais yanapaswa kutolewa saa 72 baada ya shughuli hiyo kukamilika.

Hii ina maana kuwa matokeo rasmi yatatangazwa leo, Jumatatu.

Ushindi wa Hichilema katika maeneo bunge 15 yaliyoko kwenye ngome ya Rais Lungu, pia unaashiria kuwa umaarufu wa mgombeaji huyo wa urais wa upinzani umeimarika pakubwa tangu uchaguzi uliopita wa 2016.

Katika uchaguzi huo Hichilema alishindwa na Rais Lungu kwa kura chache mno katika uchaguzi huo uliokuwa ushindani mkali.

Wafuasi wa upinzani walidai kulikuwa na wizi wa kura kumfaidi Rais Lungu.Katika uchaguzi wa Alhamisi, jumla ya wapiga kura 296,210 walishiriki katika maeneobunge yote 156.

Hii inawakilisha asilimia 71.75 ya idadi jumla ya wapigakura waliosajiliwa nchini Zambia, kulingana na Afisa Mkuu wa tume ya uchaguzi Patrick Nshindano alipowahutubia wanahabari jijini Lusaka.

Matokeo ya kwanza, ambayo yalitarajiwa kutolewa Ijumaa, yalicheleweshwa baada ya shughuli ya kuhesabu kura kujivuta.

Hii ni kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo.

Vile vile, vyama vya kisiasa vilikataa matokeo ya awali kutoka kwa eneobunge moja, ambayo yalitofautiana na yale yaliyonakilisha na waangalizi wa uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi Zambia (ZEC) iliruhusu uchaguzi kuendelea hadi saa kumi na moja jioni, siku ya Ijumaa ili kutoa nafasi kwa watu waliokuwa foleni kupiga kura zao.

Hii ni licha ya serikali kuzima mawasiliano ya intaneti kote nchini humo.

Vile vile, fujo za kisiasa ziliripotiwa katika maeneo matatu nchini.

Serikali ilidinda kutoa taarifa zozote kuhusu kuzimwa kwa mawasiliano ya intaneti, hatua ambayo watumiaji walisema pia iliathiri mitandao kadhaa ya kijamii kama vile Facebook.

Hichilema alikashifa chama tawala kwa kuamuru kuzimwa kwa mitandao ya kijamii.

Aliitaka tume ya mawasiliano nchini Zambia kufungua intaneti “ili wananchi waweze kufuatilia matangazo ya matokeo ya uchaguzi na waendelee na maisha yao bila kuingiliwa.”

You can share this post!

DINI: Lisheni akili zenu mawazo mazuri, fikra za tumaini na...

JAMVI: Misimamo mikali OKA inaweza kuwafaidi au kuwabomoa...