Habari Mseto

Kiongozi wa wasiomwamini Mungu asimamishwa kazi

January 23rd, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Muungano wa Wakenya Wasioamini uwepo wa Mungu, Bw Harrison Mumia ametishia kushtaki Benki Kuu ya Kenya kwa kumsimamisha kazi kutokana na misimamo ya kisiasa aliyoeneza kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Bw Mumia jana alikashifu hatua iliyochukuliwa kumsimamisha kazi katika Taasisi ya Mafunzo ya Kifedha ya Kenya (KSMS) inayomilikiwa na CBK.

Ilifichuka hatua za kinidhamu zilianza kuchukuliwa dhidi yake tangu mwaka wa 2017 ambapo alijitetea kwamba hakutangaza msimamo wake wa kisiasa hadharani kama ilivyodaiwa na akakata rufaa ilipokuwa imeamuliwa asimamishwe kazi.

Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa na KSMS, ilisemekana sheria za ajira serikalini zimepiga marufuku watumishi wa umma kushiriki katika shughuli za kisiasa ambazo zinaweza kufanya afisi zao kuonekana kuegemea upande mmoja wa kisiasa.

Bw Mumia jana alifichua barua tele kuhusu suala hilo na mojawapo iliyoandikwa Januari 11, 2019 na Kaimu Mkurugenzi wa KSMS, Bw Dennis Mutuku ilionyesha amesimamishwa kazi baada ya rufaa aliyowasilisha kukataliwa.

Sehemu ya barua hiyo ilisema kamati ya rufaa ilikutana Septemba 19, 2018 ndipo ikaamuliwa hakutoa maelezo yoyote mapya kupinga uamuzi uliotolewa awali.

“Hatujapata sababu yoyote ya kubadili uamuzi wa kukusimamisha kazi kwa hivyo uamuzi wa awali utatekelezwa. Kwa msingi huu, unatakiwa kuanza shughuli ya kuondoka mara moja,” ikasema.

Lakini kupitia kwa mtandao wa Twitter, Bw Mumia alijitetea kwamba maandishi ya kisiasa yaliyotegemewa kumfuta kazi hayakutoka kwake na hata kama ingekuwa ni yeye aliyaandika, hatua iliyochukuliwa ni ukiukaji wa haki za waajiriwa.

“Ninaandaa kesi dhidi ya CBK nikitaka kulipwa ridhaa. Nitashirikiana pia na wengine ili tusaidiane kupinga hatua hii ya ukiukaji wa haki zetu za kikatiba katika CBK,” akasema.