Habari Mseto

Kioni: Uhuru ndiye ‘kingpin’ wa Mt Kenya hadi kifo, Gachagua ajipe shughuli

January 9th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KATIBU Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, amesema kuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ndiye anafaa kushikilia nafasi ya msemaji wa eneo la Mlima Kenya hadi kifo chake.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatatu asubuhi, Bw Kioni alisema kuwa kwa sasa, hakupaswi kuwa na mjadala wowote kuhusu nafasi hiyo kwani Bw Kenyatta “alishaijza kitambo”.

“Kulingana nami na wenyeji wa eneo hili, hilo si jambo linalofaa kujadiliwa, kwani Bw Kenyatta ndiye kiongozi na msemaji wetu kisiasa,” akasema Bw Kioni.

Kauli hiyo inajiri huku mjadala mkali ukiendelea kuchacha kuhusu ni nani kiongozi halisi wa kisiasa wa eneo hilo, baina ya Bw Kenyatta na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Wafuasi wa Bw Gachagua wanashikilia kuwa ikizingatiwa ndiye mwanasiasa mwenye cheo kikubwa zaidi cha kisiasa serikalini kutoka eneo hilo, ndiye msemaji wake, huku wafuasi wa Bw Kenyatta wakisema bado ndiye anayeliongoza.

Kulingana na Bw Kioni, sababu ya Bw Kenyatta kutohudhuria mkutano uliopangiwa kufanyika mjini Nyeri Jumapili iliyopita ni kwamba hakukuwa na umuhimu wake kuwepo, kwani tayari ndiye kiongozi wa eneo hilo.

Mwandalizi mkuu wa mkutano huo, Bw Maina Njenga, alikuwa amesema lengo kuu la maandalizi yake ni kumtawaza Bw Kenyatta kama kiongozi na msemaji rasmi wa kisiasa wa eneo hilo.

“Bw Kenyatta hangehudhuria mkutano huo kwani hakukuwepo na mipamgo hiyo. Pili, hangetawazwa, kwani tayari ndiye kiongozi rasmi wa kisiasa,” akasema Bw Kioni.

Polisi walilazimika kuwatawanya wafuasi wa Bw Maina waliojaribu kuingia katika uwanja huo, wakiwatuhumu kuwa wa kundi la Mungiki.

Bw Gachagua pia aliwaagiza maafisa wa usalama katika eneo hilo kuzima mikutano yoyote ambayo haikuwa imeruhusiwa.

Naibu Rais alidai kuwa “anawafahamu wale wanaoandaa mikutano hiyo” japo hakutoa ufafanuzi wowote.

“Hatutawaruhusu wale wanaojaribu kulifufua kundi hatari katika eneo hili. Tunajua jinsi lilivyowafanyia ukatili watu wetu,” akasema Bw Gachagua.

Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Bw Kioni kujitokeza kudai eneo halina pengo la uongozi wa kisiasa ni ishara kwamba makabiliano makali yataendelea kushuhudiwa baina ya Bw Gachagua na Bw Kenyatta katika siku zijazo.