Michezo

Kipa aomba msamaha kwa kukubali kulimwa mabao 5

July 16th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

MNYAKAJI wa Tusker FC Patrick Matasi amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya kupokezwa kichapo kizito cha 5-2 na Kariobangi Sharks kwenye mechi ya ligi ya KPL iliyogaragazwa Jumamosi 14 kwenye uwanja wa Camp Toyoyo jijini Nairobi.

Kipa huyo  wa timu ya Taifa Harambee Stars aliyejiunga na wanamvinyo hao wakati wa dirisha la uhamisho wa wachezaji mwezi Juni 2018 kutoka Posta Rangers amekosa kuridhisha kwa kuwa amekuwa akifungwa mabao rahisi sana.

“Ilikuwa siku mbaya katika mechi dhidi ya Kariobangi Sharks siku ya Jumamosi. Nahisi masikitiko makuu miongoni mwa mashabiki na ninafahamu  ilikuwa kinyume cha matarajio ya mashabiki wetu,” akasema Matasi.

Kichapo walichopokezwaTusker FC kiliendeleza unyonge wao dhidi ya Kariobangi Sharks ambao walidumisha rekodi ya kutoshindwa na mabingwa hao wa KPL mwaka wa 2012.

Baada ya timu hizo kukutana mara nne, Kariobangi Sharks wameshinda mara mbili na kusajili sare mbili. Tusker FC hawajawahi kushinda mchuano wowote uliowakutanisha.

Hata hivyo, Matasi amewataka mashabiki hao kutoyeyusha matumaini na watarajie timu ambayo itaimarika sana zikiwa zimesalia mechi 11 kabla ligi kukamilika.

“Tunaenda kuyarekebisha makosa yetu na tunatarajia matokeo mazuri katika mechi zilizosalia. Tutashinda mechi nyingi na watafurahi tena,” akasema Matasi.

Tusker FC wanakibarua kizito dhidi ya mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka katika mechi ya ligi Jumapili 29