Michezo

Kipa Courtois aendelea kufunga mabao akitarajiwa kuitwa baba mara ya tatu

March 16th, 2024 2 min read

IMEKUSANYWA NA CHRIS ADUNGO

KIPA mzoefu wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ubelgiji, Thibaut Courtois, yuko pua na mdomo kuwa baba mzazi kwa mara ya tatu.

Hii ni baada ya mkewe, Mishel Gerzig, kutumia mtandao wa Instagram wiki hii kutangaza kuwa amesalia na miezi ya kuhesabu tu kabla ya kujaliwa kimalaika.

Kipusa huyo alikuwa amejikwatua kwa rinda fupi jeusi lililoacha nje sehemu kubwa ya mapaja na maziwa ndani ya sidiria.

Mishel, 26, alikuwa akitabasamu katika nyingi za picha alizopigwa akiwa amehudhuria hafla ya ‘Acqua Di Gio’ iliyodhaminiwa na kampuni ya Giorgio Armani jijini Madrid, Uhispania.

Demu huyo raia wa Israeli, alianza kuhusiana na Courtois mnamo 2021 na wakafunga pingu za maisha mnamo Julai 2023.

Mishel alitangaza ujauzito wake mwezi Januari huku Courtois akipangwa kuwa baba kwa mara ya tatu.

Nyota huyo ana watoto wawili kutoka kwa uhusiano wake wa awali na Marta Dominguez – Adriana, 8, na Nicolas, 6.

Mishel sasa huzingua mashabiki mara kwa mara kwenye Instagram ambapo anajivunia zaidi ya wafuasi 767,000.

Baada ya kuchapisha habari za ujauzito wake mtandaoni kwa mara nyingine, Mishel aliweka picha akiwa amevalia bikini kutoka kwenye safari ya awali ufukweni.

Chini ya picha hiyo aliweka maelezo: “Upendo wetu unakua. Hatuwezi kusubiri kukutana nawe kimalaika chetu.”

Mishel alitumia pia mtandao wake wa Instagram kulalamika kwamba fungate yao haikuenda kabisa na mipango yake kwa sababu ya ratiba ngumu ya mumewe.

“Ilikuwa tufurahie fungate jinsi ambavyo wanandoa wengine wapya hufanya baada ya harusi. Lakini yangu ilikuwa ovyo kabisa! Tulikosa muda wa hata kushiriki michezo ya siri chumbani jinsi nilivyotazamia,” akatanguliza Mishel.

“Ratiba ya Courtois isingeruhusu kamwe tufanye mambo mengi pamoja! Mazoezi ya kila mara ufuoni Ibiza yalimeza muda wake wote. Niliachwa pweke hadi ikabidi ‘niolewe’ na gilasi kadhaa za sharubati na vibanzi ili nisukume wakati,” akaongeza.

Courtois alianza kuchovya kwa Mishel baada ya kutemana na Mayka Rivera mnamo Februari 2021, mwezi mmoja baada ya kipusa Elsa Izac,43, kupasua mbarika kuhusu jinsi alivyohusiana na kipa huyo kisiri hadi wakapata mtoto wa kiume, Enzo, mnamo 2017.

Kwa mujibu wa Elsa ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wanne, Courtois alianza kumtambalia kimapenzi mnamo 2016 alipokuwa jirani yake jijini London, Uingereza. Courtois alikuwa akichezea Chelsea wakati huo.