Michezo

Kipa Jordan Pickford aambiwa hapajaharibika neno kambini mwa Uingereza

November 6th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza amesema kwamba alimpigia simu kipa Jordan Pickford baada ya gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililomshuhudia mlinda-lango huyo akimjeruhi beki matata wa Liverpool, Virgil van Dijk.

Kwa mujibu wa Southgate, nia yake ya kuwasiliana na kipa huyo wa Everton ilikuwa ni kumhakikishia kwamba nafasi yake katika timu ya taifa ingalipo.

Pickford, 26, alishtumiwa pakubwa kwa tukio hilo ambalo lilimshuhudia Van Dijk akipata jeraha baya la goti litakalomweka nje ya kampeni zote za msimu huu.

“Nilitambua jinsi alivyokuwa akishambuliwa mitandaoni na nikahisi kwamba kushtumiwa huko kungemwathiri zaidi kimawazo na kushusha kiwango cha ubora wa matokeo yake,” akasema Southgate.

“Nilimpigia hima kwa nia ya kumtuliza na kumhakikishia kwamba tukio hilo lisingemnyima nafasi katika timu ya taifa,” akaongeza.

Ingawa Pickford hakuadhibiwa kwa kosa hilo la kumchezea Van Dijk vibaya, maafisa wa polisi mjini Merseyside walianzisha uchunguzi dhidi ya madai kwamba baadhi ya mashabiki walitumia mtandao wa Twitter kumtishia kipa huyo maisha.

Gozi hilo la EPL kati ya Everton na Liverpool lilichezewa ugani Goodison Park mnamo Oktoba 17, siku chache baada ya Pickford kupangwa katika kikosi cha kwanza kilichotegemewa na Southgate dhidi ya Ubelgiji na Denmark. Pickford alikuwa sehemu ya kikosi kilichonogesha michuano hiyo licha ya kusajili msururu wa matokeo duni katika ngazi ya klabu.

Japo aliwajibishwa tena ligini katika mechi iliyowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Southampton, kipa huyo alipumzishwa dhidi ya Newcastle waliowachapa Everton 2-1 mnamo Oktoba 31, 2020.

Hata hivyo, kocha Carlo Ancelotti amesisitiza kwamba Pickford atakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kitakachotegemewa na Everton dhidi ya Manchester United katika EPL mnamo Novemba 7, 2020 ugani Goodison Park.

Mbali na Pickford, kocha Southgate amemwita pia kambini kipa Dean Henderson wa Man-United na Nick Pope wa Burnley kwa minajili ya mechi tatu zijazo dhidi ya Jamhuri ya Ireland, Ubelgiji na Iceland.