Michezo

Kipa Karius wa Liverpool ayoyomea Ujerumani kuwadakia Union Berlin

September 27th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIPA Loris Karius wa Liverpool ameingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Union Berlin kinachoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 27 alitamatisha kandarasi yake kambini mwa Besiktas ya Uturuki aliokuwa akiwachezea kwa mkopo mnamo Mei, 2020. Wakati huo, kipa huyo alikuwa akielekea kukamilisha kipindi cha kuhudumu kwake kwa mkopo kambini mwa Besiktas kwa miaka miwili.

Karius alijiunga na Liverpool mnamo 2016 baada ya kushawishiwa kubanduka kambini mwa Mainz ya Ujerumani kwa kima cha Sh658 milioni. Mechi ya mwisho kwa Karius kuchezea Liverpool ilikuwa 2018 katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Masihara ya Karius katika fainali hiyo iliyochezewa jijini Kiev, Ukraine, yalishuhudia Liverpool wakipokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa vijana wa kocha Zinedine Zidane.

Union Berlin walikamilisha kampeni za Bundesliga msimu uliopita katika nafasi ya 11 jedwalini.