Michezo

Kipa mahiri Juma Kaseja asema Tanzania inaweza kutetemesha katika Afcon

June 15th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU na MASHIRIKA

DAR, ES SALAAM, Tanzania

MLINDA lango mahiri Juma Kaseja amesema kikosi cha Taifa Stars kina uwezo mkubwa wa kupiga hatua katika michuano ya AFCON, nchini Misri.

Kaseja alisema kocha wa kikosi hicho, Emmanuel Amunike ana uwezo wa kuiwezesha timu hiyo kuiwakilisha vyema Tanzania katika michuano hiyo itakayoanza Juni 21.

“Huu ni wakati wa wananchi kuungana pamoja kuitakia mema timu yetu wakati wa fainali hizo za AFCON. Hatufai kumlaumu kocha kutokana na uteuzi wake, kwani ndiye anayeelewa ni wachezaji wa aina gani anahitaji kulingana na mfumo wake.”

“Ni jukumu la wachezaji wote kutambuwa kwamba wamebeba bendera ya taif letu, hivyo sharti wajitahidi,” alisema Kaseja ambaye aliwahi kuwa kipa wa kikosi hicho cha Taifa Stars.

Mechi ya mwisho

Baada ya kucheza na wenyeji na kushindwa 1-0, Taifa Stars itacheza mechi ya mwisho dhidi ya Zimbabwe ambayo imepangiwa katika kundi moja na DR Congo, Uganda pamoja na wenyeji Misri.

Taifa Stars imo kwenye Kundi C pamoja na Senegal Algeria na majirani Harambee Stars ya Kenya.