Michezo

Kipa Origi akoseshwa raha siku yake ya kuzaliwa akiwa michumani mwa Harambee Stars ikibwagwa na Comoros

November 16th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KIPA Arnold Origi alikuwa na siku mbaya ya kuzaliwa kwake alipofungwa mabao mawili timu ya Kenya ikibwagwa 2-1 na Comoros kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya mataifa haya mawili akisherehekea kufikisha umri wa miaka 37 hapo Novemba 15, 2020.

Mshambuliaji wa Red Bull Salzburg El Fardou Ben Mohamed aliweka wanavisiwa hao kifua mbele katika dakika ya 21.

Kiungo mshambuliaji wa FC Masr Cliff Nyakeya alisawazisha 1-1 dakika ya 36 kabla ya Faiz Mattoir kuzamisha chombo cha Kenya mapema katika kipindi cha pili.

Origi, ambaye pia ana uraia wa Norway baada ya kuishi nchini humo tangu Januari 1, 2007, alirejea michumani kudakia Harambee Stars ikitoka 1-1 dhidi ya wanavisiwa hao hapo Novemba 11.

Binamu huyo wa mshambuliaji wa Ubelgiji na klabu ya Liverpool Divock Origi alikuwa amestaafu mara mbili kuchezea Stars kabla ya kuitikia mwito wa kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee wa kurejea kikosini. Aling’ara msimu huu wa 2020 akichezea klabu ya HIFK inayoshiriki Ligi Kuu nchini Finland.

Alistaafu mwaka Februari 2012 akilalamikia kusumbuliwa na majeraha anapowajibikia taifa akitaka kumakinikia zaidi majukumu ya klabu yake ya Moss FK. Hakukaa nje sana kwani alijiunga tena na Stars iliyokuwa chini ya Francis Kimanzi mnamo Juni 2012 kabla ya mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Namibia.

Miaka mitano iliyopita, aliamua kuchukua mapumziko kutoka timu ya taifa akishughulikia uraia wa Norway,

Alikuwa na matumaini ya kuongoza Kenya kufika Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya pili mfululizo. Hata hivyo, ndoto hiyo ilipata pigo kubwa kufika Cameroon mwaka 2022 baada ya Kenya kudondosha alama tano dhidi ya Comoros.

Stars italazimika kufanya miujiza ya kupepeta Misri jijini Nairobi (Machi 22) na Togo jijini Lome (Machi 30) mwaka 2021 katika mechi zake za Kundi G zilizosalia na kuomba Misri isishinde michuano yake mitatu iliyobaki dhidi ya Togo jijini Lome hapo kesho, Comoros nchini Misri (Machi 30).

Comoros inaongoza kundi hili kwa alama nane kutokana na mechi nne ikifuatiwa na Misri iliyozoa alama tano baada ya kusakata michuano mitatu.

Kenya ni ya tatu kwa alama tatu baada kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Misri (Alexandria), Togo na Comoros (Nairobi) na kupoteza jijini Moroni. Togo inavuta mkia kwa alama moja baada ya kucheza mechi tatu.