Kipa wa Ajax apigwa marufuku ya mwaka mmoja kwa kutumia pufya

Kipa wa Ajax apigwa marufuku ya mwaka mmoja kwa kutumia pufya

Na MASHIRIKA

KIPA wa Ajax na timu ya taifa ya Cameroon, Andre Onana amepigwa marufuku ya mwaka mmoja katika masuala ya soka kwa hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alifanyiwa vipimo vya afya mnamo Oktoba 2020 na chembechembe za dawa haramu aina ya furosemide zikapatikana katika sampuli ya mkojo wake.

Hata hivyo, Ajax wamesisitiza kwamba Onana alimeza kimakosa dawa zilizokuwa za mkewe alipougua mwanzoni mwa mwezi huo wa Oktoba.

Kikosi cha Ajax na Onana wamefichua azma ya kukata rufaa kwenye Jopo la Mizozo ya Spoti (CAS) dhidi ya maamuzi hayo yaliyochukuliwa na Uefa.

Kupitia taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari, Onana alisema alimegundua kwamba alikuwa amemeza dawa zilizokuwa za mkewe kwa kudhani kwamba ni aspirin alizokuwa ameagizwa na daktari wake kutumia. Kiini cha kosa lake hilo la Onana ambaye amesema adhabu aliyopokezwa ni kubwa kupindukia, ni kushabihiana kwa boksi zilizokuwa na dawa hizo mbili – yake na ya mkewe.

“Kila mtu ni zao la makosa ya binadamu. Kila mtu anajua kwamba naishi maisha ya kiuadilifu na nimekuwa nikipinga sana matumizi ya dawa haramu za kusisimua misuli. Sidhani nahitaji kuingilia matumizi ya pufya ili kujikuza kitaaluma,” akasema Onana.

Katika taarifa yao, Ajax walisema kwamba Uefa ilikiri kuwa Onana hakukusudia kutumia pufya ila shirikisho hilo la soka la bara Ulaya likasisitiza kwamba ni jukumu la kila mwanamichezo kuhakikisha kwamba hakuna dawa zilizoharamishwa zinastahili kuingia katika miili yao.

Onana ambaye amechezea Cameroon mara 18, sasa atakosa kuwa sehemu ya kampeni zilizoahirishwa za Kombe la Afrika (AFCON) 2021. Cameroon wamepangiwa kuwa wenyeji wa fainali hizo zitakazoandaliwa Januari 2022.

Hadi alipopigwa marufuku, Onana hakuwa amefungwa bao lolote kwenye mechi 20 za Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) msimu huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kivumbi kati ya Rotich na Kinyamal mbio za Relays zikiingia...

Ghost ataja 28 kuanza maandalizi ya Harambee Stars ya AFCON...