Michezo

Kipa wa Liverpool atishiwa maisha baada ya kufanya masihara UEFA

May 28th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

MAAFISA wa polisi jijini Liverpool, Uingereza wamesema wana habari kuwa baadhi ya mashabiki wanatisha kumuua kipa wa Liverpool, Loris Karius baada ya mechi ya fainali ya Klbu Bingwa Ulaya ambayo The Reds walilimwa 3-1 na Real Madrid.

Mjerumani huyo, pamoja na familia yake wanaishi kwa hofu baada ya vitisho vya kuwaua kutokana na masihara ya kipa huyo yaliyosaidia Real kupachika mabao matatu Jumamosi usiku.

Baada ya mechi hiyo, Karius alionekana akibubujikwa na machozi huku akiwaomba radhi mashabiki ambao hawakuamini angefanya makosa kama hayo.

Vitisho vya kila aina vilijaa mitandaoni dhidi ya kipa huyo na familia yake lakini polisi wa Merseyside wakasema wanachukulia posti hizo kwa uzito na kuwa watachunguza wenye akaunti.

“Tuna taarifa kuhusu vitisho kwenye mitandao ya kijamii. Polisi wa Merseyside watawachukulia hatua kali wanaotoa vitisho hivyo. Uchunguzi unaendelea,” wakasema.

Kipa huyo alimpa straika Karim Benzema bao rahisi na baadaye akaruhusu shuti la Gareth Bale kuingia kwa neti.

Kipa msaidizi wa Liverpool Simon Mignolet alimtetea Karius akisema masihara kama hayo hutokea kwa mechi na kuwa hafai kulaumiwa kiwango cha kutishiwa maisha.