Michezo

Kipande FC yaamini ikijituma itakwea ligini

May 26th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kipande FC inalenga kujituma kwa udi na uvumba kuhakikisha ndani ya miaka mitano ijayo imefuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

Kipande FC inayonolewa na kocha, Simon Mkanzi ni kati ya timu zinazoshiriki mechi za Ligi ya Kaunti chini ya FKF Tawi la Nairobi West msimu huu.

”Tunaamini tuna kikosi imara ambapo msimu huu tunalenga kumaliza kati ya nafasi tatu bora kwenye jedwali tukijiandaa kupigania tiketi ya kusonga mbele kwenye kampeni za msimu ujao,” meneja wake, Hannington Kimathi alisema na kuongeza kwamba mwanzo wa ngoma wamepania kuanzisha timu ya wachezaji wa umri wa chini kuanzia miaka kumi.

Meneja huyo anasema timu ya wachezaji chipukizi itasaidia pakubwa kujaza mapengo baada ya wengine kutwaliwa na timu zingine kutoka kikosi cha wakubwa.

Kadhalika alidokeza kwamba lazima wachezaji hao wajitume kukabili wapinzani wao kwa kuzingatia timu zote zimejipanga kutifua vumbi kali kusaka tiketi ya kusonga mbele msimu ujao.

Alidai kwamba endapo watafaulu kupata ufadhili bila shaka kikosi hicho kitafanya vizuri zaidi kinyume na matarajio ya wengi.

Kocha wake, Simon Mkanzi anasema “Ninaamini ninao wanasoka wazuri na wenye uwezo wa kufanya kweli kwenye kampeni za msimu huu lakini lazima wakaze buti. Tunakabiliwa na ushindani mkali mbele ya timu zingine kama MAA FC na South B United kati ya zingine.”

Kipande FC ilianzishwa mwaka 2009 na wachezaji sita lakini waliendelea kuongezeka hatua kwa hatua ambapo inajivunia kusaidia wengi kujiepusha dhidi kushiriki matendo maovu mitaani.

Katika mpango mzima kocha wake ana imani tosha wataendelea kukuza wachezaji zaidi na kusajiliwa kuchezea klabu zinazoshiriki vipute vya hadhi ya juu miaka ijayo.

Kipande FC inajumuisha wanasoka kama: Stephen Gachie, Zachary Ngundi, Joseph Kimani, Fredrick Warui, Nyanger Otondi, George Ouma, Richard Ogake, Patrick Mwambua, Joseph Irungu, Calvin Akelo na Isaack Lackinoi. Pia wapo Ashford Mbugua, Julius Otondi, Martin Kimathi, Nderi Gichuru, Boniface Nduswa, Boniface Lumumba na David Nduta kati ya wengine.

Meneja huyo anashukuru wote waliwahi kujitokeza kuwapiga jeki kwenye juhudi za kuendeleza shughuli zao michezoni ikiwamo kampuni ya Betika pia mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi kati ya wengine.

Kadhalika anatoa mwito kwa wahisani kujitokeza kusaidia klabu za michezo mashinani ili kuokoa vijana wenye talanta mbali mbali kutimiza malengo yao maishani.