Habari

Kipchoge ajikwaa mbioni huku Brigid Kosgei aking'aa London

October 5th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA wamegawanyika kuhusu mshikilizi wa rekodi ya dunia Eliud Kipchoge kuduwazwa kwenye London Marathon hapo Jumapili katika siku ambayo Brigid Kosgei aliondolea mabingwa wa dunia 2015 aibu alipohifadhi umalkia wake.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Mawaziri Amina Mohamed (Michezo) na Najib Balala (Utalii) na mshambuliaji matata wa Harambee Stars Michael Olunga waliongoza orodha ndefu ya Wakenya waliomiminia Kosgei ujumbe wa pongezi.

Bw Odinga pia alipongeza Kipchoge kwa juhudi zake akishauri kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kutia vijana moyo kuwa kuteleza sio kuanguka.

Baadhi ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii hawakuelewa uhusiano kati ya sikio na ukimbiaji pale Kipchoge aliposema kwa namna fulani kufunga kwa sikio lake kulichangia katika yeye kumaliza katika nafasi ya nane.

Wakenya walikuwa na matumaini makubwa na washikilizi wa rekodi za dunia za mbio za kilomita 42 Kipchoge na Kosgei kuwa watatamba kwenye makala hayo ya 40 yaliyofanyika katika bustani ya St James’s na kupeperushwa moja kwa moja na runinga ya NTV.

Hata hivyo, Kosgei ndiye alifanikiwa katika kampeni yake akikata utepe kwa saa 2:18:58, huku bingwa wa mwaka 2015, 2016, 2018 na 2019 Kipchoge akimaliza katika nafasi ya nane.

Kabla ya kuandikisha matokeo yake mabaya kabisa kwenye marathon jijini London jana, bingwa wa Olimpiki Kipchoge alikuwa ameshinda marathon 11 zikiwemo pia Berlin (mara tatu) na Chicago na kukamilisha Berlin katika nafasi ya pili 2013 tangu ajitose katika marathon miaka minane iliyopita.

Kosgei alifuatwa na Mwamerika Sara Hall (2:22:01) aliyepiku Mkenya, bingwa wa dunia Ruth Chepng’etich (2:22:05) hatua chache kwenye laini.

Bingwa huyo wa Chicago Marathon alikuwa bega kwa bega na Chepng’etich kwa kipindi kikubwa cha mbio hizo za kilomita 42 zilizoanza giza likiwa na pia mvua ikinyesha.

Hata hivyo, Kosgei alimtoka Chepng’etich baada tu ya kufika kilomita ya 30 na kufungua mwanya mkubwa uliomsaidia sana kutwaa taji la wanawake ambalo Kenya imeshinda mara nane katika kipindi cha miaka tisa iliyopita.

Vincent Kipchumba alikuwa Mkenya wa kwanza katika kitengo cha wanaume katika nafasi ya pili nyuma ya Muethiopia Shura Kitata.

Kipchoge, ambaye ni binadamu wa kwanza kutumika mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili (1:59:40 katika INEOS1:59 Challenge), alimaliza katika nafasi ya nane (2:06:49).

“Baada ya kilomita 25, sikio langu lilifunga na halikuweza kufunguka. Hata hivyo, michezo huwa hivyo. Tunastahili kukubali kushindwa na kuangalia tunavyoweza kushinda tena,” alisema Kipchoge baada ya kubwagwa London.

Baadhi ya mashabiki hawakutaka kusikia sababu hiyo wakisema hakuna uhusiano kati ya sikio na ukimbiaji.