Michezo

Kipchoge anusia taji la kifahari la Laureus

January 17th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KWA Kwa mwaka wa pili mfululizo, nyota Mkenya Eliud Kipchoge amechaguliwa kuwania tuzo ya mwanamichezo bora duniani ya Laureus ambayo mshindi atajulikana mnamo Februari 17, 2020, jijini Berlin, Ujerumani.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya saa 2:01:39, ambaye pia ni mtu wa kwanza kutimka umbali huo chini ya saa mbili (alikimbia saa 1:59:40 kwenye mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge nchini Austria mwezi Oktoba 2019), atawania tuzo hiyo dhidi ya wanamichezo wengine watano akiwemo mwanasoka bora duniani Lionel Messi kutoka Argentina.

Mwanatenisi shapavu Rafael Nadal (Uhispania), mwendeshaji mahiri wa pikipiki Marc Marquez (Uhispania), mwanagofu mtajika Tiger Woods (Marekani) na dereva mashuhuri wa magari ya langalanga Lewis Hamilton (Uingereza) wanakamilisha orodha ya wawaniaji wa kitengo hicho cha juu.

Kipchoge, ambaye amenyakua mataji mengi tu hivi majuzi likiwemo mwanariadha bora duniani, alijumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo hiyo mwaka 2019 na kushinda kitengo cha Ufanisi wa Kipekee (Exceptional Achievement) baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya kilomita 42 kwa sekunde 78 mjini Berlin mwaka 2018.

Bingwa wa mwanamichezo bora mwanamke mwaka 2017 na 2019 Simone Biles (michezo ya sarakasi) atatumai kujiongezea taji la tatu baada ya kukutanishwa na Waamerika wenzake Allyson Felix (riadha), Megan Rapinoe (soka) na Mikaela Shiffrin (mbio za juu ya theluji (ski). Wawaniaji wengine katika kitengo hiki ni mwanariadha Shelly-Ann Fraser-Pryce (Jamaica) na mwanatenisi kutoka Japan, Naomi Osaka.

Viongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza Liverpool wameorodheshwa kuwania tuzo mbili – Timu ya Mwaka na Timu iliyorejea kwa kishindo.

Vijana wa Jurgen Klopp watawania Timu ya Mwaka dhidi ya mabingwa wa Kombe la Dunia la Wanawake Marekani, washindi wa Kombe la Dunia la raga ya wanaume ya wachezaji 15 kila upande Afrika Kusini, wafalme wa Ligi Kuu ya mpira wa vikapu nchini Marekani Toronto Raptors, mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia la mpira wa vikapu la wanaume Uhispania na timu ya magari ya mbio za langalanga ya Mercede