Michezo

Kipchoge apanga njama ya kutia Bekele adabu London

August 10th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

LICHA ya kuwa hajashindana kwa siku 300, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon za wanaume, Eliud Kipchoge anahisi yuko fiti kutetea ubingwa wake wa London Marathon hapo Oktoba 4.

Bingwa huyu wa Olimpiki anajivunia kutwaa mataji ya London mwaka 2015, 2016, 2018 na 2019. Anasema hatadharau mpinzani yeyote akiwemo hasimu wake mkuu Kenenisa Bekele kutoka Ethiopia.

Kipchoge anasema kuwa mazoezi yake wakati huu ambapo michezo bado imepigwa marufuku nchini Kenya yamemfanya kuwa imara hata zaidi.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliarifu wanahabari hapo Jumamosi kupitia mtandao kuwa miezi miwili ijayo itakuwa muhimu zaidi katika mazoezi yake kwani itaamua utayarifu wake.

“Nimezamia mazoezi kwa zaidi ya miezi mitatu sasa. Niko katika hali nzuri, lakini nitakuwa hata bora miezi miwili ijayo kukutana na washindani wengine mjini London,” alisema binadamu huyo wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili (1:59:40), katika Mbuga ya wanyamapori ya Maasai Mara akizungumza na Waziri wa Utalii Najib Balala.

Bingwa huyo mara tatu wa Berlin Marathon, ni balozi wa sekta ya utalii wa Kenya.

Kivumbi kati yake na bingwa mtetezi wa Berlin Marathon, Bekele kinasubiriwa kwa hamu kubwa. Kitakuwa kivutio kwa mbio za London Marathon mwaka huu.

Wakimbiaji hawa wanajivunia muda ya kasi ya juu katika mbio hizo za kilomita 42.

Kipchoge anashikilia rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 aliyoweka akitwaa taji la Berlin Marathon mwaka 2018 huku Bekele akikosa kuifikia rekodi hiyo kwa sekunde mbili tu mwaka jana.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 za wanawake, Mkenya Brigid Kosgei pia anatarajiwa kuwa katika orodha ya kinadada watakaowania taji la London Marathon 2020.

Orodha ya wawaniaji itakuwa ndogo (40) ili kuzuia maambukizi ya virusi hatari vya corona vilivyosababisha makala haya ya 40 kuahirishwa kutoka Aprili hadi mwezi Oktoba.

Wakimbiaji watazunguka eneo la St James’s Park mara 19.8 kabla ya kumalizia mbio hizo katika sehemu ya kawaida ya The Mall.

Orodha kamili ya wakimbiaji watakaoshiriki London Marathon mwaka huu bado haijatolewa.