Kipchoge apigwa jeki na INEOS kutimka kwenye marathon Olimpiki 2024

Kipchoge apigwa jeki na INEOS kutimka kwenye marathon Olimpiki 2024

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge (pichani) hana mpango wa kustaafu hivi karibuni.

Hii ni baada ya kusaini mkataba wa muda mrefu na kampuni ya kemikali ya INEOS utakaoshuhudia akielekea jijini Paris, Ufaransa mwaka 2024 kutetea taji lake la Olimpiki.

Bingwa huyo wa marathon katika Olimpiki za 2016 na 2020, ni binadamu wa kwanza na pekee kuwahi kukamilisha umbali huo chini ya saa mbili.

Akishirikiana na INEOS katika mbio maalum za INEOS1:59 Challenge mwaka 2019, Kipchoge, ambaye sasa ana umri wa miaka 37, alitimka kilomita hizo 42 kwa saa 1:59:40 jijini Vienna, Austria.

Muda huo haukutambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani kwa sababu alikimbia pekee yake akisaidiwa na wawekaji kasi waliobadilishana kwa zamu.

“Kupokea usaidizi kutoka kwa kampuni hiyo kubwa ni motisha kubwa kwangu na wenzangu. Tumekuwa na ushirikiano mzuri tangu tuanze kufanya kazi pamoja na tayari tumebadilisha ulimwengu pamoja. Nafurahia kuendelea kuimarisha rekodi mbalimbali,” alisema Kipchoge atakayekuwa mtu wa kwanza kuzoa mataji matatu ya marathon kwenye Olimpiki ikiwa akifanikiwa jijini Paris.

Kwa sasa, anashikilia rekodi ya mataji mawili katika umbali huo kwa pamoja na Mjerumani Waldermar Cierpinski na Muethiopia Abebe Bikila.

  • Tags

You can share this post!

Dada 2 matatani kwa kukeketwa

Uchungu wa mama

T L