Habari Mseto

Kipchoge aponyoka kesi ya ufisadi

November 16th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Ijumaa aliambia mahakama ya kupambana na ufisadi kwamba hatamshtaki bingwa mbio za riadha ulimwenguni Kipchoge Keino kwa ufisadi uliokumba michezo ya OIimpiki mjini Rio De Jeneiro mwaka wa 2016.

DPP kupitia kwa Bi Emily Kamau alimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti kwamba hatamfungulia mashtaka Bw Keino ya matumizi mabaya ya mamlaka ya ulaghai wa Sh17.5 bilioni.

“Kama nilivyoeleza mahakama mwezi uliopita kuwa DPP ameagiza uchunguzi mpya ufanywe kumhusu Bw Keino, sasa imebainika hakufanya makosa na atakuwa shahidi wa Serikali,” alisema Bi Kamau.

Wakili Cecil Miller aliyemwakilisha Bw Keino alithibitisha kuwa Bw Keino hatafunguliwa mashtaka mbali atakuwa shahidi katika kesi inayomkabili Balozi wa Kenya nchini Austria ambaye pia alikuwa Waziri wa Michezo Bw Hassan Wario.

Bw Wario, aliyekuwa katibu mkuu Bw Richard Titus Ekai , Bw Haroun Komen Chebet, aliyekuwa kinara wa timu iliyowakilisha Kenya katika michezo hiyo Bw Stephen Kiptanui arap Soi , Bw Patrick Kimathi Nkabu na aliyekuwa katibu wa kamati ya olimpik Bw Francis Kinyili Paul walishtakiwa upya kwa kashfa hiyo ya Sh55milioni.

Mawakili Mabw Miller, Julius  Kitheka, Bosesk Kimutai, George Kanyi na Bi Emmy Chelule walilalamika kwamba afisi ya DCI  haijawapa nakala za mashahidi.

Awali kiongozi wa mashhtaka ya umma alikuwa amesema kusikizwa kwa kesi hakutaendelea kwa vile “mawakili wanaowatetea washtakiwa hawakuenda kupokea nakala za mashahidi.”

Lakini mawakili Miller,  Kitheka, Kimutai, Kanyi na Chelule walimweleza hakimu mkuu Douglas Ogoti, “DPP anadanganya. Tumeenda katika afisi ya Mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) na kuelezwa nakala za taarifa za mashahidi haziko tayari.”

Bw Miller alisema , “Nilipiga simu na kuenda mwenyewe na sikupewa nakala hizi. Namtetea Bw Ekai , aliyekuwa katibu mkuuu wizara ya spoti na sasa ndiye Balozi wa Kenya nchini Urusi.”

Bw Kitheka alisema ameenda katika afisi hiyo mara tatu na kuelezwa nakala za mashahidi haziko tayari.

Bw Ogoti alimwuliza afisa anayechunguza kesi hiyo , “Kati ya kiongozi wa mashtaka nani anasema ukweli?”

“Je, nakala hizo zilikuwa tayari wakati mawakili walifika katika afisi yako kuzichukua? Niambie ukweli.”

“Nakala hizo hazikuwa tayari lakini sasa ziko tayari na ziko kwa gari katika egesho. Nitawapa nakala hizo baada ya kutajwa kwa kesi hii,” afisa huyo alijibu.

Bw Ogoti alitahadharisha  viongozi wa mashtaka kuwa hatasita kuwachukulia hatua kwa vile ni mahakama inayolaumiwa kwa kutoendelea na kesi na kumbe inakoseshwa na maafisa wa DCI ambao hawatekelezi maagizo ya korti.

Bw Wario na wenzake Mabw  Ekai, aliyekuwa kiongozi wa timu ya Kenya kwenda Rio kwa michezo ya OIimpik 2016 Stephen Soi , katibu mkuu wa kamati ya olimpik nchini Kenya (Nock) Francis Kinyili Paul, aliyekuwa afisa mkuu masuala ya fedha wizara ya spoti Patrick Kimathi Nkabu na aliyekuwa mkurugenzi wa masuala ya usimizi Bw Haron Komen Chebet walikanusha mashtaka 17 ya matumizi mabaya mamlaka yaliyopelekea Serikali kupoteza Sh55milioni.

Walikanusha mashtaka dhidi yao. Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa tasilimu.

Kesi itatajwa Desemba 6, 2018 mawakili waeleze ikiwa walipokea nakala za mashahidi.