Michezo

Kipchoge ayoyomea Uholanzi kukutana na wasimamizi wake

October 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon, Eliud Kipchoge aliteua kusafiri hadi Uholanzi kukutana na wasimamizi wake katika makao makuu ya Global Sports Communications huku Wakenya wengine walioshiriki naye London Marathon wakirejea nyumbani mnamo Oktoba 6, 2020.

Kipchoge, ambaye alipania kutwaa taji la tano la London Marathon mwaka huu, aliambulia nafasi ya nane katika makala ya 40 ya mashindano hayo mnamo Oktoba 4, 2020 baada ya kupata tatizo la sikio katika hatua ya kilimota 25.

Mwethiopia Shura Kitata aliibuka mshindi wa mbio hizo kwa upande wa wanaume baada ya kumpiku Mkenya Vincent Kipchumba katika hatua ya mwisho. Kitata aliyetwaa ubingwa wa London Marathon kwa mara yake ya kwanza, alifika utepeni baada ya saa 2:05:41, sekunde moja pekee mbele ya Kipchumba.

Kwa mujibu wa Kipchumba, kosa alilolifanya ni kuchomoka mapema katika dakika chache za mwisho na hivyo kuishiwa pumzi sekunde chache kabla ya Kitata kumpita na kuwa wa kwanza kuufikia utepe.

“Ninafurahia matokeo yangu japo ningalishinda mbio hizo iwapo ningalimpigia Kitata hesabu mapema. Nilichomoka mapema na kumpa Kitata fursa ya kuongeza kasi na hatimaye kuibuka mshindi,” akasema Kipchumba ambaye ni mshindi wa Amsterdam Marathon, Uingereza.

“Tulianza mbio vizuri licha ya kwamba hali ya hewa ilikuwa mbovu. Ilinilazimu kusalia katika kundi la kwanza lililokuwa likiongoza mbio hizo baada ya kuona Wakenya wenzangu wakisalia nyuma na baadhi yao kujiondoa. Japo Waethiopia walijaribu kila ujanja kunipiku, nilisalia imara hadi dakika za mwisho.”

“Tulipoondoka Kenya kuelekea London, kulikuwepo na joto jingi sana. Lakini mambo yalikuwa tofauti asubuhi ya kuamkia mbio. Mvua kubwa ilinyesha na baridi ya kutisha,” akaeleza Kipchumba ambaye ni mkazi wa Chepkatet, Eldoret.

Kipchumba, ambaye ni mwanakikosi cha 2Running Club mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi, alimtakia Kipchoge ambaye pia ni bingwa wa Olimpiki kwenye mbio za kilomita 42, afueni ya haraka.

Vivian Cheruiyot, ambaye hakukamilisha mbio hizo za London Marathon kwa upande wa wanawake, alikataa kuzungumza na wanahabari pindi kikosi cha Kenya kilipowasili katika uwanja wa ndege wa Eldoret.

Cheruiyot aliibuka mshindi wa London Maratho mnamo 2018 kabla ya kuambulia nafasi ya pili mnamo 2019.

Wanariadha wengine wa Kenya waliorejea nchini kutoka London, Uingereza ni Edith Chelimo, Marius Kipserem na Benson Kipruto. Bingwa wa dunia katika marathon, Ruth Chepng’etich, ambaye aliambulia nafasi ya tatu jijini London, alisalia jijini Nairobi huku Brigid Kosgei aliyehifadhi taji lake la London Marathon akisalia nchini Uingereza.

Wanariadha hao ambao kwa pamoja na wenzao waliowawekea kasi jijini London, walisafiri hadi Nairobi kwa ndege ya British Airways kabla ya kuunganisha safari hadi Eldoret kwa kupitia ndege ya Jambojet.

Kosgei alikuwa mwingi wa sifa kwa Vivian Kiplagat aliyemwekea kasi ya kutosha jijini London.

“Mashindano hayo hayakuwa rahisi. Nilijua Ruth Chepng’etich alikuwa mshindani mkali. Niliongeza kasi na kumwacha kwa mita kadhaa ili asisome hatua za miguu yangu. Vivian (Kiplagat) aliondokea katika hatua ya kilomita 25 na kuniachia kazi rahisi iliyosalia,” akasema Kosgei ambaye hutiwa makali na kocha Eric Kimaiyo.