Kipchoge, Chepng’etich roho mkononi tuzo ya manariadha bora ikiandaliwa

Kipchoge, Chepng’etich roho mkononi tuzo ya manariadha bora ikiandaliwa

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Eliud Kipchoge, Faith Chepng’etich na Emmanuel Wanyonyi watafahamu Jumatano usiku kama walifanya ya kutosha kushawishi mashabiki na Shirikisho la Riadha Duniani kutawazwa washindi wa mwaka 2021.

Shirikisho la Riadha Kenya (AK) pia linawania tuzo ya shirikisho bora.

Bingwa mara mbili wa Olimpiki mbio za kilomita 42 Kipchoge, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya saa 2:01:39, anawania tuzo ya mwanariadha bora mwanamume dhidi ya Joshua Cheptegei (Uganda), Ryan Crouser (Amerika), Mondo Duplantis (Uswidi) na Karsten Warholm (Norway).

Kipchoge, 37, ambaye majuzi alitawazwa mwanamichezo bora wa Olimpiki 2020, aliibuka mwanariadha bora duniani mwaka 2018 na 2019. Mrukaji wa kutumia fito Duplantis ndiye bingwa mtetezi.

Chepng’etich,27, anawania kuwa mwanariadha bora mwanamke dhidi ya Sifan Hassan (Uholanzi), Sydney McLaughlin (Amerika), Elaine Thompson-Herah (Jamaica) na bingwa wa 2020 Yulimar Rojas kutoka Colombia.

Bingwa wa dunia mbio za mita 800 za washiriki wasiozidi umri wa miaka 20 Wanyonyi, 17, anawania tuzo ya chipukizi anayeinuka kwa haraka mwanamume. Wapinzani wake ni Sean Burrell (Amerika), Erriyon Knighton (Amerika), Tadese Worku (Ethiopia) na Sasha Zhoya (Ufaransa). Keely Hodgkinson (Uingereza), Silja Kosonen (Finland), Christine Mboma (Namibia), Athing Mu (Amerika) na Zerfe Wondemagegn (Ethiopia) wako katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya chipukizi anayeinuka kwa haraka mwanamke.

Mmoja kutoka orodha ya mashirikisho ya riadha ya AK (Afrika), Czech (Ulaya), Costa Rica (Amerika Kaskazini na Kati na Caribbean), Ecuador (Amerika ya Kusini) na Japan (Asia) atatazwa shirikisho bora 2021. Hafla ya kutuza wanariadha itaandaliwa jijini Paris, Ufaransa na kupeperushwa kupitia mitandao ya YouTube na Facebook ya Shirikisho la Riadha Duniani.

You can share this post!

Msiwape sikio wanaofanya siasa za ukabila, Gavana Mvurya...

Chebukati sasa akataa ‘kupangwa’

T L