Kipchoge kurejea Ujerumani kujiandaa kwa Hamburg Marathon

Kipchoge kurejea Ujerumani kujiandaa kwa Hamburg Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MFALME wa mbio za kilomita 42 duniani, Eliud Kipchoge ametangaza atarejea mjini Hamburg nchini Ujerumani mnamo Aprili 11.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, bingwa huyo wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya umbali huo ya saa 2:01:39 alisema kuwa atarejea katika mji huo alikoanzia utimkaji wa mbio za kilomita 42 mwaka 2013.

“Narudi nilikoanzia maisha yangu ya kukimbia mbio za kilomita 42. Hapa ndipo yote nimefanya katika marathon yalianzia,” alisema Kipchoge mnamo Alhamisi.

Aliongeza, “Natumai kuwapa motisha watu wengi kote duniani kwa kukimbia mbio za kufana katika barabara za mji huo mzuri.”

Kipchoge alifichua mpango huo wake saa chache baada ya timu yake ya NN Running pia kuthibitisha kuwa mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 36 atakuwa katika orodha ya zaidi ya watimkaji nyota 100 watakaowania ubingwa wa Hamburg Marathon.

Timu hiyo ilitangaza ushirikiano na waandalizi wa Hamburg Marathon juma lililopita kuandaa mbio hizo katika eneo ambalo washiriki pekee wataruhusiwa.

Taarifa kutoka Ujerumani zinasema kuwa mbio za Hamburg Marathon zitakuwa muhimu kwa Kipchoge kufuta machozi ya kupoteza taji la London Marathon mwezi Oktoba 2020 na pia kutoa fursa kwa wakimbiaji wanaotafuta tiketi ya kuwakilisha mataifa yao kwenye Michezo ya Olimpiki 2020 jijini Tokyo mwezi Julai/Agosti mwaka huu.

Kipchoge alishinda Hamburg Marathon mwaka 2013 kwa saa 2:05:30 ambayo inasalia kuwa rekodi ya mbio hizo za Hamburg. Alikamilisha Berlin Marathon katika nafasi ya pili kwa saa 2:04:05 baadaye mwaka huo.

Kutoka hapo, Kipchoge alifagia mataji 10 katika marathon katika miji ya Rotterdam nchini Uholanzi, Chicago (Amerika) na London (Uingereza) mwaka 2014.

Alishinda London Marathon kwa mara ya pili mwaka 2015 na Berlin Marathon kwa mara ya kwanza mwaka 2016 ambao pia aliongeza taji la Olimpiki mjini Rio de Janeiro, Brazil. Alitikisa tena mijini Berlin na London mwaka 2017 na 2018.

Pia, alijaribu kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili mjini Monza nchini Italia mwaka 2017 alipoandikisha 2:00:25 kabla ya kutimiza azma hiyo mjini Vienna, Austria alipomaliza mbio maalum za INEOS1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 mnamo Oktoba 2019.

Katika mwaka 2020 uliovurugwa na mkurupuko wa virusi vya corona, Kipchoge alishiriki mbio moja pekee akimaliza London Marathon katika nafasi ya nane mnamo Oktoba 4 kwa saa 2:06:49.

  • Tags

You can share this post!

Maafisa wa kaunti motoni kwa kupatikana na silaha

Akamatwa akijaribu kuhonga maafisa wa KDF