Michezo

Kipchoge mawazo na moyo wake wote ni Olimpiki pekee

April 18th, 2024 2 min read

AYUMBA AYODI na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa zamani wa rekodi ya mbio za wanaume za kilomita 42, Eliud Kipchoge, amesimamisha shughuli zake zote kumakinikia kutetea taji lake la Olimpiki kwenye makala ya 33 jijini Paris, Ufaransa mnamo Julai 26 hadi Agosti 11.

Kipchoge, 39, ambaye ametawala marathon katika makala mawili mfululizo, pia alieleza kuwa mwelekeo hasi na ukabila vinaumiza taifa, lakini akasema kuwa wanamichezo wanaweza kurekebisha hali.

Hata hivyo, Kipchoge, ambaye ameshinda mbio 16 kati ya 20 ambazo ameshiriki, amesema kuwa nafasi yake si salama katika kikosi cha Olimpiki kwa sababu watimkaji wenzake wanne wana uwezo.

Kikosi cha wanaume cha Kenya kina Kipchoge, bingwa wa Tokyo Marathon Benson Kipruto na nambari mbili wa Tokyo Marathon Timothy Kiplagat, mshindi wa medali ya fedha ya Berlin Marathon Vincent Kipkemoi na bingwa wa Prague Marathon Alexander Mutiso.

“Naamini kwamba nitafuzu kushiriki Olimpiki kwa mara yangu ya tano na hiyo ndiyo sababu naweka akili yangu yote, moyo wangu na mawazo yangu katika matayarisho,” akasema Kipchoge anayelenga kuwa mwanamume wa kwanza kunyakua mataji matatu mfululizo ya marathon kwenye Olimpiki.

“Hiyo ndiyo sababu sitajihusisha na shughuli nyingine mpaka nifike Paris,” akafichua Kipchoge akikiri kuwa ushindani mkali bado upo si tu kutoka kwa wakimbiaji wa Kenya, bali pia Ethiopia, Uganda na Amerika, miongoni mwa wengine.

Kipchoge alikuwa akizungumza katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi wakati wa sherehe za Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) za kuadhimisha siku 100 kabla ya Olimpiki 2024.

“Kuna ushindani kila mahali, huku wanariadha kutoka mataifa 106 wakitarajiwa kushiriki. Kila mtu ana nafasi sawa ya kuibuka na ushindi na ni mshindi kivyake. Itakuwa kujidanganya kupuuza yeyote,” akasema Kipchoge aliyekamata nafasi ya 10 kwenye marathon yake ya mwisho jijini Tokyo, Japan mwezi uliopita.

Heshima

“Kila mara nitawapa heshima wapinzani wangu kwa sababu huu ni mchezo ambao kila mtu anajituma vilivyo akatarajia ushindi,” alieleza Kipchoge, akisema kuwa ni kupitia tu ushirikiano Kenya itapata ushindi mwingine.

Kipchoge alionya Wakenya dhidi ya laza damu na kutarajia miujiza kwa hivyo lazima wafanye bidii ndiposa wafaulu.

Aidha, marehemu Kelvin Kiptum, ambaye alishinda London Marathon 2023 kwa saa 2:01:25, atakumbukwa wakati wa London Marathon 2024 hapo Aprili 21.

Washiriki wapiga makofi kwa sekunde 30 na pia video ya maisha ya Kiptum kuchezwa kabla ya mbio hizo kuanza.

Kiptum alifariki pamoja na kocha wake Gervais Hakizimana katika ajali mbaya Februari 11 mjini Eldoret. Alivunja rekodi ya Kipchoge ya saa 2:01:09 akishinda Chicago Marathon 2023 kwa 2:00:35.