Michezo

Kipchoge na Brigid safu ya mbele kutwaa Tuzo za IAAF

November 13th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAKENYA wanapigiwa upatu wa kutamalaki tuzo za Wanariadha Bora wa Mwaka Duniani kwa mara nyingine, katika hafla itakayoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) baadaye mwezi huu jijini Monaco.

Bingwa wa Dunia na Olimpiki katika mbio za masafa marefu, Eliud Kipchoge, atapania kutetea taji lake kwa upande wa wanaume.

Kipchoge alivunja rekodi ya dunia katika mbio hizo za marathon mwaka 2018 na kutawazwa Mwanariadha Bora wa Kiume 2018.

Caterina Ibarguen wa Colombia ambaye ni bingwa wa dunia katika fani ya kuruka mbali, ndiye alitia kapuni taji la Mwanariadha Bora wa Kike 2018, baada ya kumpiga kumbo Mkenya Beatrice Chepkoech.

Hadi kutuzwa kwa Kipchoge mnamo 2018, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 David Rudisha, alikuwa ndiye Mkenya wa pekee kuwahi kuibuka Mwanariadha Bora Duniani aliponyakua taji la 2010.

Tuzo hizo za wanariadha bora wa mwaka zilianzishwa mnamo 1988. Tuzo za mwaka huu zitaandaliwa Novemba 23 mjini Monaco, Ufaransa.

Kipchoge aliweka historia Oktoba 12, 2019, kwa kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili aliposhiriki kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge jijini Vienna, Austria. Alikamilisha kivumbi hicho katika muda wa saa 1:59:40.2.

Kati ya washindani wakuu wa Kipchoge mwaka huu ni Mkenya Timothy Cheruiyot, aliyetwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye mashindano ya Riadha za Dunia hivi majuzi jijini Doha, Qatar.

Cheruiyot aliyetawazwa bingwa wa Diamond League mnamo 2017, 2018 na 2019, pia amewahi kunyakua nishani ya fedha kwenye mbio za mita 1,500 wakati Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

Wawaniaji wengine ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 800, Donavan Brazier wa Amerika; Mmarekani Christian Coleman, ambaye ni mfalme wa mbio za mita 100; Joshua Cheptegei wa Uganda, aliye bingwa wa dunia katika mbio za nyika na mita 10,000; Steven Gardiner wa Bahrain, mbio za mita 400; Sam Kendricks wa Amerika, kuruka kwa ufito; Noah Lyles wa Amerika, mbio za mita 200; Daniel Stahl wa Uswidi, urushaji kisahani; na Karsten Warholm wa Norway, ambaye ni bingwa wa dunia mbio za mita 400 kuruka viunzi.

Wakenya Brigid Kosgei, Hellen Obiri na Beatrice Chepkoech wameorodheshwa kuwania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.

Kosgei aliingia kwenye orodha hiyo baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya marathon upande wa wanawake, katika mbio za Chivago. Kwenye mbio hizo za Oktoba, Kosgei alinyoa dakika moja na sekunde 21 kutoka kwa rekodi ya zamani iliyokuwa imedumu miaka 16.

Nyota huyo alikamilisha mbio za Chicago Marathon nchini Amerika kwa muda wa saa 2:14.04, na kuondoa rekodi ya Mwingereza Paula Radcliffe ya saa 2:15:25 aliyowekwa 2003.

Chepkoech ndiye bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji. Kando na kutia kapuni ubingwa wa mbio za Diamond League msimu huu, mwanadada huyo alitawala mashindano saba kati ya manane aliyoshiriki mwaka huu. Muda wa dakika 8:57.84 alioandikisha katika Riadha za Dunia jijini Doha, ulimvunia nishani ya dhahabu. Kiini cha kuteuliwa kwa Obiri ni ufanisi aliojivunia katika Mbio za Nyika za Dunia jijini Aarhus, Denmark, mapema mwaka 2019.

Kisha kunyanyua medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 5,000 katika Riadha za Dunia za Doha, kwa muda wa dakika 14:26.72. Awali, alikuwa amesajili muda bora wa dakika 14:20.36 katika mbio hizo jijini London, Uingereza, mnamo 2017.

Chepkoech ndiye anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, kwa muda wa dakika 8:44:32. Aliweka rekodi hiyo wakati wa mbio za Diamond League mjini Fontvieille, Monaco, nchini Ufaransa. Kwenye mbio hizo za Julai 2018, Mkenya huyo alifuta rekodi ya Mbahrain Ruth Jebet kwa sekunde nane. Kwa rekodi hiyo mpya, Chepkoech alikuwa mwanamke wa kwanza kabisa kutimka mbio hizo chini ya dakika 8:50 na dakika 8:45.

Obiri, Kosgei na Chepkoech watatoana jasho na Shelly-Ann Fraser-Pryce wa Jamaica ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 100,. Vile vile, kuna Mwingereza Katarina Johnson-Thompson (heptathlon) na Sifan Hassan wa Uholanzi, anayeshikilia ubingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 na mita 10,000.