Michezo

Kipchoge na Cherono kupokelewa kishujaa JKIA

September 17th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limefichua Jumatatu kwamba linapangia mabingwa wapya wa mbio za Berlin Marathon Eliud Kipchoge na Gladys Cherono mapokezi ya kishujaa.

Kipchoge,33, alivunja rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 kwa kushinda makala ya 45 kwa saa 2:01:39. Alifuta rekodi ya Mkenya mwenzake Dennis Kimetto ya saa 2:02:57, ambayo pia iliwekwa jijini Berlin mwaka 2014. Cherono, 35, alivunja rekodi ya Berlin Marathon ya wanawake iliyoshikiliwa na Mjapani Mizuki Noguchi tangu mwaka 2005 ya saa 2:19:12. Alikata utepe kwa saa 2:18:11.

Katika mahojiano ya simu, Rais wa AK, Jackson Tuwei ameambia tovuti ya Swahili Hub kwamba wanafanya mipango kabambe kuhakikisha mabingwa hao wa Berlin Marathon mwaka 2015, 2017 na 2018 wanapokolewa kwa heshima kubwa.

“Bado hawajatuarifu kuhusu mipango yao ya kurejea nchini (saa na tarehe), lakini tunasubiri wapumzike kidogo halafu tuwasiliane nao. Walifanya kazi ngumu na nzuri jijini Berlin.

Kama AK tumepanga kuwapa mapokezi mazuri kuwashukuru kwa kazi hiyo safi. Tunajua watu wengi (serikali, makampuni na mashirika mbalimbali) wangependa kujiunga nasi katika sherehe ya kuwapokea kwa hivyo hatutaki kufungia mtu yeyote nje,” amesema Tuwei jijini Nairobi.

Kipchoge na Cherono walizawadiwa Sh5.5 milioni kwa kunyakua mataji. Cherono aliongezwa Sh4 milioni kwa kuvunja rekodi ya Berlin Marathon.

Bingwa wa Olimpiki Kipchoge atapokea karibu Sh6.9 milioni kwa kuvunja rekodi ya dunia kutoka kwa waandalizi wa Berlin Marathon. Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) pia hutuza washikilizi wa rekodi za dunia.

Vilevile, Kipchoge atapokea donge nono kutoka kwa wadhamini wake kampuni ya kuunda vifaa vya michezo Nike pamoja na kampuni ya magari ya Isuzu Kenya, ambayo imemfanya kuwa balozi wake wa magari ya aina ya Isuzu D-Max.

Waandalizi pia huwapa wanariadha watajika marupurupu ya kuitikia mwito wa kushiriki mashindano yao.