Michezo

Kipchoge na Wanja kushiriki mradi wa uhamasishaji wa kamati ya Olimpiki Nock

June 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge na seta wa timu ya taifa ya voliboli ya wanawake almaarufu Malkia Strikers, Janet Wanja wanatarajiwa leo Alhamisi usiku kuhamasisha wanamichezo wa humu nchini.

Mbali na kuwashauri kuhusu namna ya kusimamia raslimali zao, Kipchoge na Wanja watawaelekeza jinsi ya kuhusiana na vyombo vya habari na kujidhibiti baada ya mafanikio yao katika fani mbalimbali kuwafanya watu watajika katika jamii.

Wawili hao watakuwa wawasilishaji wa mwisho katika msururu wa makongamano ambayo yamekuwa yakiendeshwa na Kamati Kuu ya kitaifa ya Olimpiki (Nock).

Kwa mujibu wa Francis Mutuku ambaye ni Katibu Mkuu wa Nock, wawili hao ambao wametawala fani zao kwa kipindi kirefu, watawapa wanamichezo wenzao siri nyingi za ufanisi na jinsi ya kuongoza maisha ya kitaaluma huku wakisalia kutangamana vyema na wanajamii wengine.

“Ni muhimu sana kuhamasisha wanamichezo kuhusu umuhimu wa makuzi ya kijumla maishani. Kadri wanavyozidi kupata sifa na mafanikio tele, baadhi ya wanamichezo hupotoka kimaadili, hujitosa katika uovu, hupuuza familia zao na kufuja mali,” akatanguliza Mutuku.

“Badala yake, tunatumia majukwaa haya kuwaelekeza wanamichezo wetu vilivyo, kuwashawishi kuwekeza katika sekta mbalimbali za maendeleo na kuinuana maishani,” akasema.

Hadi kufikia sasa, wanamichezo ambao wamehusishwa na Nock katika mradi huo ni John Ngugi ambaye ni bingwa mara tano wa dunia katika mbio za nyika na mshindi wa Olimpiki katika mbio za mita 5,000 mnamo 1988, nahodha wa zamani wa Harambee Stars Musa Otieno na bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake, Hellen Obiri.

Wengine ni aliyekuwa mfungaji bora wa muda wote wa trai katika raga ya dunia Collins Injera na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za nusu marathon, Geoffrey Kamworor.

Nock imepania kutumia kipindi hiki cha janga la corona kutalii mbinu mbalimbali za kuimarisha ulingo wa michezo kwa kuhusisha washikadau mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa maoni anuwai kupitia majadiliano ya mitandaoni.