Habari

Kipi kitarajiwe bajeti ikisomwa?

June 13th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KATIKA makadirio ya bajeti mwaka wa fedha 2019/2020 ajenda kuu nne ni miongoni mwa nguzo zinazolengwa ili kufanikisha maendeleo.

Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa Henry Rotich leo Alhamisi anatarajiwa kusoma bajeti hiyo inayokadiriwa kuwa ya kiasi cha Sh3.02 trilioni.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akipigia debe uafikiaji wa ajenda hizo.

Aidha, amekuwa akisafiri katika mataifa mbalimbali ya kigeni kwa minajili ya kuvutia wawekezaji, pamoja na kuimarisha uhusiano mwema wa kibiashara, lengo likiwa kuzifanikisha.

Ajenda hizo ni kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini, kuwepo kwa matibabu bora na nafuu kwa wote, ujenzi wa viwanda na uundaji wa makazi bora na ya bei nafuu.

Katika makadirio ya bajeti mwaka huu wa kifedha, uundaji wa viwanda unapaniwa kupokea mgao wa Sh125.4 bilioni huku ajenda ya makazi Sh103.2 bilioni.

Kulingana na taarifa ya waziri Rotich kuhusu bajeti hii sekta ya afya itapokea Sh82.8 bilioni.

Takriban kaunti 10 zimekumbatia mfumo huo, ikiwemo Laikipia, Kirinyaga, Nyeri, Kisumu na Taita Taveta. Zingine ni Nyandarua, Machakos, Nakuru, Nairobi na Makueni.

Sekta ya kilimo na ambayo ndiyo uti wa mgongo wa taifa hili pamoja na ukuaji wa mashambani na mijini, itapokea mgao wa Sh59.1 bilioni.

Waziri Henry Rotich akitarajiwa kusoma makadirio ya bajeti, wakulima wanaendelea kulalamikia bei ghali ya pembejeo hususan mbegu, mbolea na dawa za magonjwa na wadudu.

Kulingana na John Muthee, kutoka Laikipia, anasema baada ya kuondoa gharama ya matumizi katika kilimo, mkulima anasalia na mapato kiduchu.

“Tunachoomba ni bajeti iangazie gharama ya kulima, ili Wakenya wawe na motisha ya kuzalisha chakula,” anasema Muthee.

Hata ingawa wengi wamekumbatia utumiaji wa mbolea ya mifugo, ile ya kisasa ingali ghali.

“Mfuko wa kilo 50 unagharimu zaidi ya Sh3,000. Mimi ni mkulima wa mahindi, gunia la 90 nikinunuliwa chini ya bei ya Sh3,000 ni faida ninapata au hasara?” anashangaa Bw Lawi Kimeli kutoka Uasin Gishu, aliyezungumza na Taifa Leo.

Usafirishaji wa mazao kwa baadhi ya wakulima umekuwa kizingiti kwa sababu ya barabara duni na zisizopitika.

Daniel Kihara, mkulima Lari kaunti ya Kiambu, analalamikia barabara mbovu hasa msimu wa mvua. “Hukuza mimea inayovunwa baada ya miezi mitatu. Msimu wa mvua barabara humu hazipitiki, mazao huozea shambani,” anasema Kihara.

Ili kufanikisha bajeti ya mwaka huu, halmashauri ya utozaji ushuru nchini KRA inatarajiwa kuchangia Sh2.2 trilioni zitakazokusanywa kutoka kwa walipa ushuru.

Pia Sh289.2 bilioni zinapaniwa kuchangwa humu nchini na Sh607.8 bilioni kutoka mataifa ya kigeni kupitia mikopo. Kufikia sasa mataifa ya kigeni yanadai Kenya deni Sh5.12 trilioni.