Michezo

#KipKeinoClassic: Vanice Kerubo aibuka mshindi wa mbio za mita 400 kuruka viunzi

October 3rd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Michezo ya Afrika 2019 Vanice Kerubo ameibuka mshindi wa mbio za mita 400 kuruka viunzi katika kitengo cha kitaifa cha mbio za kimataifa za Kip Keino Classic zinazopeperushwa moja kwa moja na runinga ya NTV uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Jumamosi.

Kerubo alinyakua medali ya dhahabu kwa urahisi baada ya kukamilisha mzunguko huo mmoja wa viunzi 10 kwa dakika 1:02.29. Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 18 alifuatwa zaidi ya sekunde mbili nyuma na Caroline Waiganjo (1:04.82) naye akazoa nishani ya shaba Elizabeth Kimuyu (1:06.09).  Kitengo hiki kilivutia wakimbiaji wanane, wote wakiwa ni Wakenya.

Mashindano haya yamevutia wanariadha 700 kutoka zaidi ya mataifa 30. Haya ni makala ya kwanza kabisa ya mashindano haya yaliyotajwa Kip Keino Classic kwa heshima ya jagina Dkt Kipchoge Keino,80, aliyekuwa katika orodha ya Wakenya wa kwanza kufanya vyema kwenye riadha miaka ya 60 na 70.

Duru ya Kip Keino Classic ni ya kufunga msimu wa makala ya kwanza kabisa ya Riadha za Dunia za Continental Tour zilizoanzishwa na Shirikisho la Riadha Dunia (World Athletics) mwaka 2020.