Michezo

Kipkorir bingwa wa Athens Marathon

November 11th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

John Komen Kipkorir aliendeleza ubabe wa Kenya katika mbio za kilomita 42 za Athens nchini Ugiriki baada ya kunyakua taji la mwaka 2019 kwa saa 2:16:34, Jumapili.

Katika mbio hizi zilizokimbiwa katika mvua na maeneo ya milima, Komen, 42, alimpita Felicien Muhitira kutoka Rwanda zikisalia mita 600 na kutwaa taji.

Ushindi huu wa Athens Marathon ni wa Kenya wa 16 tangu mwaka 2001. Ni mwaka wa nne mfululizo mwanamume kutoka Kenya alitwaa taji la Athens Marathon baada ya Luka Rotich (2016), Samuel Kalalei (2017) na Brimin Kipkorir (2018).

Hapo Jumapili, Muhitira, 25, aliridhika katika nafasi ya pili kwa saa 2:16:43 naye Mgiriki Konstantinos Gkelaouzos (2:19:02) akafunga mduara wa tatu-bora.

Eleftheria Petroulaki alishinda taji la wanawake kwa saa 2:39:00. Mkenya Shelmith Nyawira alikuwa ameshinda taji hili mwaka 2018.

Washiriki 60,000 kutoka zaidi ya mataifa 100 walihudhuria makala haya ya 37 wakiwemo 20,041 katika mbio za kilomita 42.

Matokeo (Novemba 10):

John Komen Kipkorir (Kenya) saa 2:16:34

Felicien Muhitira (Rwanda) 2:16:43

Konstantinos Gkelaouzos (Ugiriki) 2:19:02

Daniel Muteti Muindi (Kenya) 2:21:39

Khamis Bakari (Morocco) 2:23:36

Panayiotis Karaiskos (Ugiriki) 2:26:28

Charalampos Pitsolis (Ugiriki) 2:27:31