Michezo

Kiprop ashinda Vienna City Marathon kwa mara ya tatu

April 7th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NANCY Kiprop ametwaa taji la mbio za Vienna City Marathon kwa mwaka wa tatu mfululizo baada ya kushinda makala ya 36 kwa rekodi mpya ya saa 2:22:12 nchini Austria, Jumapili.

Kasi ya Mkenya huyu ni dakika moja na sekunde 35 bora kuliko rekodi ya awali ya saa 2:23:47 ambayo Mwitaliano Maura Viceconte amekuwa akishikilia tangu Mei 21 mwaka 2000.

Kiprop, ambaye alishinda mbio hizi za kilomita 42 jijini Vienna mwaka 2017 na 2018, amefuatwa kwa karibu katika nafasi ya pili na tatu na Wakenya wenzake Angela Tanui na Maurine Chepkemoi ambao pia wameandikisha muda yao bora ya saa 2:25:37 na 2:26:16, mtawalia.

Naye Vincent Kipchumba amerejesha taji la Vienna City Marathon nchini Kenya ambalo Mmoroko Salaheddine Bounasser alikuwa ametwaa mwaka 2018.

Kipchumba amekata utepe kwa saa 2:06:56 akimaliza mbele ya Mswizi Tadesse Abraham (2:07:24) na Mganda Solomon Mutai (2:08:25). Zaidi ya watimkaji 41, 000 kutoka mataifa 110 walishiriki makala haya.